CHINA na Tanzania ni nchi ambazo zimekuwa na urafiki, undugu na ushirikiano wa kina tangu enzi za waasisi Mwenyekiti Mao Zedong na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Urafiki huu umeendelea kudumishwa na viongozi wengine wote wa pande zote mbili waliofuatia baada ya waasisi hao, na kuendelezwa hadi katika ngazi ya wananchi wa China na Tanzania.

Unaweza kujiuliza ni kwa nini Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kuchaguliwa mara mbili na Rais Xi Jinping, jibu ni kwamba China inaithamini sana Tanzania, kwani pande hizi mbili zimekuwa marafiki wa kutegemeana ambao hawajahi kuangushana au kuvunjana moyo kwa namna yoyote ile.

Hivi majuzi rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alifanya ziara hapa nchini China, baada ya kualikwa na rais wa China, Xi Jinping.

Ziara hii ilipokelewa kwa furaha na shauku kubwa hasa kwa Watanzania wakijua kwamba thamani yao ni kubwa mbele ya Wachina na kwamba kutakuwa na fursa nyingi zinazohitaji kuchangamkiwa ili kuleta maendeleo ya pande mbili.

Mara ya kwanza wakati Xi Jinping anaingia madarakani kama rais mwaka 2013, nchi ya kwanza kabisa kuichagua kuitembelea katika bara la Afrika ilikuwa Tanzania.

Na sasa miaka kumi baadaye, baada ya kuchaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kwenye Mkutano Mkuu wa 20 wa CPC uliomalizika hivi karibuni tu, pia ameamua kuichagua tena Tanzania kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuja China kufanya ziara yake ya kikazi.

Hapa tunajifunza nini, tunachojifunza ni kwamba Tanzania kuwa wa kwanza mara mbili, huu ni ukweli usiopingika kuwa uhusiano baina ya nchi hizi umefika katika ngazi ya juu kabisa.

Lakini kubwa zaidi ni kwamba mimi nikiwa kama Mtanzania ambaye nimeishi hapa China kwa miaka mingi tu, naweza kusema hii ni fursa kubwa sana kwetu Watanzania kwa ujio wa rais Samia hapa Beijing.

Kwa sababu naelewa kuwa Wachina ni watu ambao hawana hiyana, na ni watu wanaopenda nchi zote hususan za Afrika ziendelee kwa pamoja bila kumwacha yeyote nyuma.

Kwenye mkutano Mkuu wa 20 wa CPC uliomalizika hivi majuzi rais Xi Jinping ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CPC alisema China itazidisha na kupanua ushirikiano wa kimataifa wenye usawa, uwazi na ushirikiano, na kudhamiria kupanua muunganiko wa maslahi na nchi nyingine.

Haya ndio maslahi anayoyazungumzia rais Xi kwa nchi za nje, kwani kwenye ziara yake mama Samia hapa Beijing, kuna mengi yaliyojadiliwa na mikataba ipatayo kumi na tano ya ushirikiano wa pande mbili katika sekta mbalimbali imefungwa, zikiwemo biashara, uwekezaji, ushirikiano wa maendeleo, uchumi wa kidijitali na maendeleo ya kijani. Haya ndio matunda makubwa ya ushirikiano huu.

Kwa sasa Watanzania nao wataendelea kunufaika na soko la China baada ya kulifungua kwa ajili ya maparachichi na pia kwa bidhaa za uvuvi zikiwemo mabondo ya samaki na minofu ya samaki.

Tunafahamu kuwa Tanzania ni nchi ya kilimo cha parachichi ambayo yanalimwa katika mikoa kadhaa, na kwa muda mrefu imekuwa ikisumbuka kutafuta soko la uhakika.

Baada ya China kufungua milango yake ya soko, ambalo linatambulika duniani kuwa ni kubwa zaidi, sasa bidhaa hii itakuwa inaletwa moja kwa moja bila kupitia upande wa tatu.

Tanzania inakuwa nchi ya pili kufunguliwa soko la parachichi ambapo hapo awali tulikuwa tukiwaonea wivu wenzetu Wakenya kwani wao wametangulia kutumia soko hili la China kuleta maparachichi yao.

Mimi ni Mtanzania ambaye natokea visiwani, Zanzibar, na tunafahamu kuwa watu wa visiwani huwa wanajishughulisha sana na ukuzaji wa uchumi wa buluu.

Ziara ya mama Samia pia itawafaidisha hata wale wanaoendesha shughuli za baharini, kwani kwa mujibu wa mikataba iliyosainiwa, China pia imefungua soko lake kwa kuuzwa bidhaa kama samaki.

Na habari njema ni kwamba baada ya makubaliano hayo kufungwa tu, kampuni kubwa ya China Alibaba iliwasiliana na balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki, wakitaka waunganishwe moja kwa moja na wauzaji wa mabondo ya samaki kutoka Tanzania ili waanze mazungumzo ya biashra.

Kwa hiyo kwa maoni yangu, ziara hii imekuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania lakini pia imewahamasisha Wachina kushirikiana zaidi na Tanzania katika mambo ya kilimo na uvuvi na mengineyo.

Natarajia kuwa huu utakuwa ni mwanzo tu kwani uchumi wa buluu pia una mapana yake, kuna bidhaa nyingi zinalimwa baharini ambazo pia zinahitajika kwenye soko la China, zikiwemo mwani, majongoo ya pwani n.k.