NA ASIA MWALIM. 

KILIMO cha mwani ni moja ya kilimo kilichopewa msukumo mkubwa na serikali kiasi kwamba kinawapa mtisha wakulima wa zao hilo.

Uongozi wa serikali ya awamu ya nan echini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Hussein Ali Mwinyi, imeweka vifaa na fedha maalumu kwa ajili ya wakulima wa zao hilo hivyo kuathiri shughuli za maendeleo ya wakulima hasa wanawake.
Pamoja na uwezeshaji huo ni ukweli usiopingika kuwa kwa muda mrefu sasa bei ya mwani imekua changamoto visiwani Zanzibar, ikilinganishwa na maeneo mengine yanayolimwa zao hilo, hivyo kuathiri maendeleo ya wakulima.

HALI YA UZALISHAJI WA MWANI ZANZIBAR

Zanzibar ni nchi ya nne 4 duniani kati ya nchi zinazozalisha mwani (Mwekundu) ikiongozwa na nchi ya Indonesia, Filipino na Malaysia, ambapo mwaka 2021 Zanzibar imezalisha takriban tani 12,000.

Kilimo cha Mwani ni moja kati ya shughuli za uchumi wa buluu, kabla ya dhana hiyo hadi wakati huu watu wanaoishi pembezoni mwa bahari wamejiajiri, kati yao asilimia 80 ni wanawake.

Ukulima wa mwani hutegemea maji ya bahari kama ukulima wampunga unavyotegemea mashamba ya ardhi, wanawake hutumia fursa hiyo kujiajiri baada ya kutambua fursa za uchumi zilizopo baharini.

ULIMAJI NA UVUNAJI WA MWANI
Mwani unalimwa na kuvunwa siku 45 hadi 60, kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa, Zanzibar huendelezwa shughuli hiyo kwa kiasi kikubwa ambapo zaidi ya watu elfu ishirini na tano (25, 000) wanalima mwani katika vijiji 86, vijiji 50 Unguja, 33 Pemba.

Baadhi ya vijiji vinavyolimwa mwani Zanzibar ni Paje, Pwani Mchangani, Bwejuu, Uzi, Jambiani, Dimani na Kisakasaka.

HUTUMIKA KWA CHAKULA
Mwani hutumika kama chakula na kutengeneza bidhaa mbali mbali ikiwemo sabuni, juice, mafuta, kashata, vileja, keki, jamu na bidhaa nyengine, ambazo zinatumiwa ndani na nje ya nchi.

Makala haya yatazungumzia kuhusu harakati za ukulima wa mwani Zanzibar, na jinsi bei inavyoathiri shughuli za kimaendeleo ya wakulima wa mwani wanawake.

TAFITI YA ZAO LA MWANI ZANZIBAR

Kwa mujibu wa utafiti wa serikali mwaka 2006 kuhusu sensa kupitia Idara ya maendeleo ya Uvuvi na Mazao baharini, kupitia Kitengo cha mwani umeonesha kuwa Zanzibar inawakulima, wa mwani zaidi ya Ishirini na tatu elfu miasaba, kati yao wanawake elfu kumi na saba miasaba na arobaini na wanaume ni elfu tano miatisa na sitini.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Tuko kwelini, Muungoni, Riziki Haji Makame, alisema changamoto kubwa inayowakabili wakulima wanawake ni bei ndogo ya mwani Shilingi miasaba 700, haikidhi mahitaji hata kilo ya mchele, waliomba serikali kuangalia namna ya kuengeza bei angalau ifike shilingi elfu mbili, ili kupunguza ukali wa maisha.

Aidha walisema wakulima wa Zanzibar wanauza kilo moja ya mwani shilingi 700, ambapo nchi nyengine Mwani mnene wanauza baina ya shilingi 2,000 hadi 2,500, mwani mwembamba wanauza 1,200 hadi 1,500.

“Shughuli za bahari ni ngumu, bei haikidhi ukilinganisha uzito wa shughuli tunazofanya baharini tunatamani tukae nyumbani.” alisema.

Alisema takribani masaa tisa wanayatumia baharini kufanya shughuli hiyo na hakuna mafanikio makubwa waliyoipta zaidi ya robo ya mahitaji yao, na baadhi ya wanawake wamesitisha shughuli za ukulima.

Mwenyekiti huyo alieleza matarijio yao baada ya kusikia sera ya Mh. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ahadi alizotoa kwa wakulima, kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu aliomba serikali iangalie kuharakisha suala hilo kwa maslahi ya wakulima.

Aidha alisema familia zinawategemea wanatamani viongozi kusikia kilio chao na kupatiwa ufumbuzi wa mabadiliko ya bei, baadhi ya wanawake wameacha kazi hiyo na kukaa majumbani kwao baada ya kukosa faida.

Aidha alisema kuanzishwa kituo cha serikali kununua mwani, kutarahisisha uhakika wa uuzaji wa mwani, kuwaunganisha wakulima na wanunuzi ili kuondoa madalali kupata faida, pia itasaidia wakulima kuuza bei moja na mahala sahihi.

Mkulima alieleza kikundi hicho kimeundwa miaka 20 iliyopita, lakini mafanikio ni madogo, pesa wanayoipta wanalazimika kuwalipa wasaidizi wanaosafisha na wanaobeba kutoka Pwani kupeleka majumbani.

Alisema katika kutafuta mabadiliko ya bei wamechukua jitihada ya kufikisha kilio chao kwa viongozi mbali mbali ikiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Maryam Mwinyi alipokutana na wakulima wa mwani eneo la kisonge hivi karibuni.

WANAVYOZUNGUMZA WAKULIMA
Mwanaisha Makame, Katibu wa kikundi cha Mwani Furahia wanawake Paje, alisema wanawake ndio viongozi katika kilimo cha mwani wanapigania  kupanda bei ya zao hilo, kwa wadau, taasisi na viongozi mbali mbali wa serikali.

Mkulima huyo alisema kilio chao zaidi katika kampuni zinazonunua mwani Zanzibar,  haiendani na gharama ya kilimo chenyewe na thamani ya zao hilo, wanatumia zaidi ya shilingi laki moja, kukamilisha mavuno ya awamu 4 na faida hupata mwisho wa mwaka.

Ombi lake kwa serikali kupitia kampuni ya mwani ni kununua zao la mwani, kama wanavyonunua karafuu kutoka kwa wakulima, pia kuweka bei maalumu ili kuweka ushindani.

Nae Mkulima Haula Hassan, kutoka Kikungwi alisema, wakulima wa mwani hawathaminiwi, wanadharaulika, mara nyingi wanaume hawataki biashara hiyo ya  utumwa. Naye Mwenyekiti wa wakulima wa mwani Zanzibar, Pavu Mcha Khamis, aliwasisitiza wakulima wa mwani kuendelea kusubiri, tayari malalamiko hayo yamefikishwa kwa viongozi, alishauri kampuni zinazonunua mwani kuhakikisha unakuwa safi,kwa uzoefu wake baadhi ya wakulima wanajenga tamaa.

Aidha alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kuanzisha kampuni ya mwani ya serikali ambayo itasimamia zao hilo ili kuondokana na madalali wanaojinufaisha. Mbali na hayo alishauri serikali kutokaa muda mrefu katika kununua mwani na badala yake kujipanga na kununua mwani huo kwa bei nzuri ili kunufaika na zao hilo na kunufaisha wakulima wa mwani.

MAMLAKA YA CHAKULA ZANZIBAR
Mkaguzi wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA), Mwajuma Kombo Ali, alisema mwani unatumika kama chakula unahitaji sehemu salama, wakulima kuacha tabia ya kuanika mwani chini, kutumia makuti, na kuacha kufanya shughuli hiyo kimazoea, aliwasisitiza kabla ya matumizi kupeleka zao hilo ZFDA, kufanyiwa uchunguzi kwa ajili ya Afya za watumiaji.

KAMPUNI ZA MWANI WAZUNGUMZA

Afisa uvuvi idara ya Uvuvi na Mazao baharini, Mondy Christopher Muhando, alisema Idara inawanasaidia wanawake kulima mwani, mwaka 2020 Zanzibar ilizalisha takriban  tani elfu 10, aliwashauri wakulima walioacha kulima mwani kuendelea, kulima zao lenye viwango bora kuondoa changamoto ya bei.

Meneja Manunuzi Kampuni ya Zanea, Justina Japhet, alisema mara nyingi bidhaa ya mwani wanaipata ikiwa katika ubora mdogo, hulazimika kutoa gharama nyengine kwa ajili ya kufanyia matayarisho kabla ya kuuza.

Alisema changamoto ya bei sio kwa maeneo yote, baadhi ya maeneo Zanzibar wanauza mwani shilingi 5000 badala ya elfu mbili, kutokana na usafi na ubora wa zao hilo, ni vyema wakulima kuanika mahala salama ili kupata mwani safi na viwango vinavyohitajika soko la dunia.

Meneja Justin alisema, kampuni ya Zanea ipo tayari kuengeza bei kulingana na uhalisia wa mwani na kuzingatia wanazingatia usafi na kiwango bora chenye uhitaji zaidi kwa wateja wao.

Akizungumzia changamoto ya bei, Mkurugenzi wa Kampuni ya mwani SM Rashid, Sleiman Mohammed Rashid, akizungumza katika kikao cha wadau wa mwani, kilichofanyika ZURA hivi karibuni alisema, wamepokea wazo la kupandisha bei bidhaa hiyo tayari wanalifanyia kazi, ingawa wanakwamishwa na baadhi ya vikwazo vya tozo na kodi kutoka serikali.

Mkaguzi Mkuu wa ndani Ofisi ya Kampuni ya mwani, Bimkubwa Omar Said, alisema serikali imechukua maoni ya wadau na wakulima wa mwani, inaendelea kupanga mikakati ya muda mrefu hatua kwa hatua.

Aidha alisema kuengeza thamani ya zao hilo ni jambo la kimkakati, tayari wameandaa mipango ya kupata zao bora, sambamba na kuwahakikishia wakulima kununua mwani kama ilivyo bei ya nchi za nje.

Nae Katibu wa Taasisi ya wakulima hai, Semeni Mohammed Salum, aliwataka wakulima kutumia teknelojia inayofanana kuanika zao hilo ili kutengeneza mnyororo wa thamani kwa kuimarisha usafi ili kupata zao lenye viwango vyenye kukubalika katika soko la dunia na kupata bei kubwa.

Mwenyekiti wa Kongano bunifu la Mwani Zanzibar (ZASCI) Dk. Flower Msunya, amewataka wakulima wa mwani kuanika bidhaa hiyo kwenye maeneo mazuri ili kupata zao lenye ubora litakalo uzwa ndani na nje ya nchi kwa bei kubwa.

Alisema matarijio yao ni kuona zao hilo linakua namba moja kuingiza mapato hapa nchini kuliko sekta nyengine na kuwaokomboa wakulima hasa wanawake.

Alifahamisha kuwa Mwani hutumika kama chakula na kutengeneza bidhaa mbali mbali, wanapaswa kutumia teknelogia wanazopatiwa bila ya kuharibu mazingira ili kupata mabadiliko ya bei.

SHIRIKA LA CHAKULA DUNIANI (FA0)
Afisa Miradi Shirika la Chakula Duniani (FAO) Leila Miraji Kihwele, alisema FAO kwa kushirikiana na Taasisi nyengine ipo tayari kushirikiana na serikali katika kuboresha zao la mwani nchini.

Alisema ili zao la mwani lipate thamani zaidi ni vyema kuekwa katika mazingira salama ya kuanikia na kuhifadhi vizuri, kuanzia kuvunwa hadi kuuzwa, ili wakulima kufaidika sawa na wakulima wa nchi nyengine.

Alisema FAO kwa kushirikiana na wizara husika itaangalia namna ya kujenga chanja kulingana na idadi ya wakulima na kiwango cha uzalishaji katika maeneo husika, kwani ukaushaji kwa njia safi na salama itathibitika zao hilo kuuzwa kwa gharama kubwa zaidi katika soko la dunia.

Mkurugenzi Mkuu kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO) DK. Masoud Mohammed Rashid, alisema kampuni hiyo inatarajia kununua mwani wa Spinosam na Kotoni kwa bei kubwa, tofauti na ya sasa ili kutekeleza dhamira ya serikali ya kuwaenua wananchi wake kiuchumi kupitia sekta ya uchumi wa bluu.

Alieleza kuwa watazingatia kuona faida zinapatikana pande zote, sambamba na kuwataka kampuni zinazonunua mwani kuangalia namna ya kupata bei nzuri na kujenga uaminifu.

Aidha alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kampeni zake alitoa ahadi kwa wakulima ikiwemo kuwainua kiuchumi, kuwatafutia masoko hivyo kuongeza bei ni moja ya ahadi zake.

HALI YA UZALISHAJI MWANI ZANZIBAR
Akizungumzia uzalishaji wa zao hilo, alisema mwaka 2021 zaidi ya tani 10,000 zililimwa na mwaka 2015/2016 tani 15,000 zillimwa, wakulima kuendelea kulima mwani, Serikali itanunua mwani kwa bei kubwaa baada ya kiwanda kinachojengwa kukamilika.

“Serikali imenaza ujenzi wa kiwanda cha mwani huko Chamanagwe uwezo wake kuchakata mwani zaidi ya tani 30000 kwa mwaka wajitahidi kulima mwani mwingi zaidi kiwanda kipate mwani wa kutosha, “alisisitiza.

Katibu Mkuu wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Aboud Suleiman Jumbe, alisema wanawake wanachukua nafasi kubwa katika uchumi wa buluu, hutumia fursa hiyo katika shughuli za usarifu na uvuvi, pia wanawake wapo mstari wa mbele katika soko la uzalishaji kwa asilimia 90.

Katibu alifahamisha kuwa suala la mwani linahitji viwanda vya kuchakata na kutengeneza bidhaa za mwani, kwa wakati huu serikali inafatilia kwa karibu ujenzi wa kiwanda cha mwani Chamanagwe Pemba, ambacho kitarahisisha maendeleo ya wanawake na wavuvi kiujumla.

Alisema mwani ni soko lenye fursa kubwa ulimwenguni, wataalamu wa soko la mwani ulimwengu wamekiri kufikia thamani ya dola binioni 15, katika kuhakikisha wanawake wanaendeleza kilimo hicho watapatiwa boti 500 kufika maji ya kina kirefu zaidi kupata mwani kwa wingi.

WAZIRI WA UCHUMI WA BULUU NA UVUVI ZANZIBAR
Akizungumza katika kikao cha warsha ya mwani kilichofanyika Agosti 8 mwaka huu ukumbi wa ZURA, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Suleiman Masoud Makame, alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane, moja kati ya Vipaombele vyake ni kuendeleza zao hilo kwa kutambua umuhimu wa zao hilo.

Alisema kwa muda mrefu wanaelewa changamoto zinazowakabili wakulima wa mwani ikiwemo suala la bei, serikali inafanya tathmini na tafiti kuona zao hilo linakwenda kutumika zaidi ya bidhaa zilizozoleka ikiwemo kutengeneza dawa, zitakazotumika kwa tiba ya binaadamu na viumbe vyengine bila ya kemikali kama nchi nyengine.

Alieleza kuwa Serikali imeweka mkazo kwenye sekta ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, inatoa elimu kwa wavuvi, kugawa vifaa, zaidi imeanza ujenzi wa kiwanda cha mwani Chamanagwe, ambacho kinataraijwa kufunguliwa January 2023.

Waziri Masoud alisema wamekusuduia kuwezesha wakulima wa vikundi kwa kuwapa mashine za kusagia mwani ambapo unga wa mwani wa kotonii utauzwa shilingi elfu kumi (10,000) badala ya elfu mbili (2000).

Aliwasisitiza wadau mwani wa Zanzibar kufanya tafiti na kuwaunga mkono wakulima wa mwani kwani wadau kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Korea, Ufaransa wanatamani kusaidia shughuli za uchumi wa buluu ikiwemo sekta ya mwani.

Aliwahakikikisha wazalishaji, wasarifu, wauzaji na wanunuzi zao hilo kutengeneza thamani kufikia mazao makuu ya biashara hapa nchini, na kuwawezesha siku hadi siku ili wapate maendeleo yao kufikia hatua ya wafanyabiashara wakubwa.

ILANI YA UCHAGUZI YA CCM. 

Katika kuendeleza zao hilo Zanzibar, Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 2050 imeeleza kuzingatia matakwa ya maendeleo endelevu ya vizazi vya sasa na vikavyo, kuweka uhakika na usalama wa chakula na kutekeleza mikakati ya kuondoa umasikini.

Pia imebainisha kuenua hali za maisha, vipato vya wananchi pamoja na haki za jamii za ushiriki wao kikamilifu katika uchumi wa buluu, ambapo Mwaka 2020 Zanzibar iliweka sera maalumu ya usimamizi wa uchumi wa buluu, ambayo ilitiwa saini October 2020.

DIRA 

Kwa kutambua shughuli za wakulima wa mwani, Dira ya mpango wa maendeleo endelevu ya Zanzibar ya mwaka 2020_2050 imeeleza, kupitia matumizi sahihi ya bahari chini ya mikakati ya muelekeo wa uchumi wa buluu ni kupatikana faida ya ajira na kupunguza umasikini kwa watumiaji wa rasilimali hiyo .

Aidha dira imeiweka uchumi wa buluu kama sekta muhimu ya kiuchumi ambayo itaufanya uchumi wa Zanzibar kuwa endelevu.

Dira hiyo inakwenda sambamba na malengo ya 14 na 6 ya agaenda ya bara la Afrika 2063, ambayo inasisitiza matumizi mazuri na endelevu ya bahari katika kuleta maendeleo.