NA ASIA MWALIM
KWA miaka ya hivi karibuni kesi za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto zimeongezeka ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
Matukio ya ukatili na udhalilishaji yanaripotiwa siku hadi siku kutokana na mchango mkubwa unaofanywa na serikali, taasisi zisizo za kiserikali pamoja na wanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kutoka ndani na nje ya nchi. Makala haya yatazungumzia jinsi wanaharakati, wanavyosimamia kundi la wanawake wajane na watoto kupata haki zao.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka kwa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa serikali Zanzibar kesi 97 za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia zimeripotiwa Juni 2022, waathirika wanawake 12 (sawa na asilimia 12.4) na Watoto 85 (sawa na asilimia 87.6).
Aidha mwaka 2020, matukio 1,363 yameripotiwa ambapo waathirika wa matukio hayo walikua wanawake 217(asilimia 15.9) na watoto 1146 (sawa na asilimia 84.1).
Taarifa, zimaeleza kuwa matukio ya ukatili na udhalilishaji waathirika wakuu ni wanawake na watoto, wahusika wa kufanya matukio hayo ni wanaume wa ndani ya familia, watu wa karibu na hata wapita njia.
WANAWAKE WAJANE.
Idadi ya wajane imefikia elfu kumi na sita (10,006) kwa Unguja na Pemba, imehusisha wanawake walioachika kwenye ndoa au mume kufariki.
Bimkubwa Khamis Sleiman (29) mjane mwenye watoto 3, alisema wanawake hasa wale waliokosa kazi rasmi wanaelemewa na mzigo wa maisha kwa kuachiwa malezi ya watoto bila ya huduma kutoka kwa waliokua waume zao.
Alisema baada ya kuachika ndoa ya kwanza, alifika kwa wazazi wake na hakupata msaada wowote wa kudai mali zake, wala matunzo ya watoto.
Alieleza kuwa awali hakuwa na uelewa wowote wa kudai haki zake na baada ya kupata elimu kutoka kwa wanaharakati, alifika Mahakamani kudai haki zake stahiki ikiwemo chakula na matibabu ya watoto.
“Nakumbuka nilipokua ndani ya ndoa nilimpatia kiasi cha fedha mume wangu kwa ajili ya mahitaji yetu, lakini ndoa ilipovunjika hakunipa chochote zaidi ya mateso, na alinilazimisha kurudisha mahari, “alisikitika.
Kupitia mateso wanayopata wanawake wajane na watoto, alishauri wanaharakati, kutoa muongozo kwa jamii ili ndoa zinapovunjika kila mmoja apate haki yake.
Maryam Shaaban Ramadhan (26) ameachika ndoa 2, amejaaliwa watoto 2, alisema kupitia Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) amepata elimu ya sheria juu ya kupata haki zake kwa baba watoto wake na sasa anapatiwa huduma za watoto.
“Lightness Bernard (42) alisema waliishi maisha ya pamoja na mzazi mwenzake zaidi ya miaka 8, walipotengana alimlazimisha kuacha baadhi ya mali zake” alisema.
Alisema hajafika kwa mwanaharakati wala sehemu yoyote kupeleka malalamiko hayo, kwani hakuwa na uelewa wa kusimamia haki zake na kufika kwa wanaharakati.
Alifahamisha kuwa viongozi wanapaswa kutoa elimu hiyo kwa upana zaidi ili kuwapunguzia mzigo wa malezi wanawake wanaoachika na kukosa mahala pa kutegemea.
Alitaka kupeleka malalamiko hayo kwenye vyombo vya sheria alihofia uchumi wake na hakubahatika kufika kwa wanaharakati” alisema.
JUMUIYA WA WAJANE ZANZIBAR (ZAWIO)
Mkurugenzi wa Taasisi ya Wajane, Tabia Makame Mohammed alisema, alipata wazo la kufungua taasisi hiyo mwaka 2019, baada ya kuona wajane wengi wanakosa mueleko wa maisha.
Tabia aliwasisitiza wanawake wanao koseshwa haki zao za msingi kufika kwenye vyombo vya sheria ikiwemo Mahakamani ili kupatiwa ufumbuzi na sio kukata tamaa au kuchukua maamuzi magumu yasiofaa.
Alisema kutokana idadi ya wajane iliyofika (elfu kumi na sita) na wengi wao kukosa huduma muhimu aliona haja ya taasisi hiyo kutoa muongozo wa ujasiriamali kwa lengo la kuwawezesha wajane, kujikimu na hali ngumu ya kimaisha.
Sambamba na hayo aliwataka wanawake kuacha utegemezi wajishughulishe kufanya kazi na kumiliki kipato chao, itawasadia kuacha kudharaulika, kunyanyasika na kupata mahitaji ya watoto na familia zao.
TAMWA
Takwimu kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, (TAMWA) Zanzibar zinaonesha kuwa kesi 230 za Ukatili dhidi ya wanawake na watoto ziliripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Julai 2021.
Aidha katika kupigania haki za wajane malalamiko 1, 600 ya talaka yaliwasilishwa katika Ofisi ya kadhi Zanzibar kutoka Chama Cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) ili wajane kupatiwa haki zao stahiki.
Mashauri 48 ya kesi za wanawake kudai haki zao na watoto yalipelekwa Ofisi ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) kati ya Januari na Juni 2021.
VIONGOZI WA DINI
Mrajisi Mahakama ya Kadhi Zanzibar, Sheik Iddi Said alisema, katika kuwasaidia wanawake na watoto kupata haki zao sheria ya dini ya kiislamu ipo wazi kutoa haki zote za wanawake na watoto hata walionyimwa matunzo.
Alisema jamii inatakiwa kuwa na uelewa wa haki zao, pia mwanamke yeyote anaekabiliwa na tatizo la kukosa mali zake, matunzo ya watoto anatakiwa kufungua kesi Mahakamani na kupatiwa muongozo sahihi.
“Tunaendesha na kusimamia kesi hizo kwa sheria namba9 ya mwaka 2007 ndio inaongozana na tafsiri ya kesi hizo” alisema.
Alieleza kuwa wastani wa kesi 1000, elfu moja zinazohusu madai ya wanandoa hupokelewa na kufunguliwa mashitaka kwa mwaka.
Aliitaka jamii hasa wanawake kuwa na utaratibu wa kuthibitisha ushirika wa mali wanazochuma pamoja kwenye ndoa, kwani Mahakama haina upendeleo wala ubaguzi kwa kuangalia jinsia za watu.
“Nimefanikiwa kusikiliza kesi 3 za mgawanyo wa mali, wanaume wanadai hawakupewa mali walizochuma na wake zao ingawa haikuwa sahihi kama walivyo dai” alisema.
Mchungaji Yohana Madai, kutoka Kanisa la The Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) alisema, kwa mujibu wa imani ya dini ya kikristo, wanandoa hawaruhusiwi kuachana, endapo itatokea ni kutokana na hali tete. (kutishiwa kifo).
Alisema sio agh-labu kutokea kesi za udhalilishaji wa kijinsia, hasa kwa ndoa zilizofungwa kanisani kutokana na elimu wanayopewa kabla na baada ya ndoa pia mali za wanandoa zinakua za pamoja kutekelezewa majukumu yote ya familia ikiwemo matunzo ya watoto.
ZAFELA
Mkurugenzi wa Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jamila Mohammed alisema, ipo haja kwa wadau wa kupinga Udhalilishaji kwa wanawake na watoto ili kupata jamii huru bila ya vitendo hivyo.
Alisema wamechukua jitihada mbali mbali za kupambana na vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kutoa elimu kwa jamii, aliwashauri wazazi kulipa uzito suala la usalama wa watoto wao kwa kukaa nao karibu na kuzungumza nao mara kwa mara.
ZAFELA, inatoa msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto ili kuhakikisha wanapatiwa haki zao.
Aidha allisema chama hicho kinatoa elimu kwa jamiii juu ya kupambania haki zao kwa mujibu wa sheria.
Kwa mwaka 2021 ZAFELA imepokea takribani malalamiko 200 ya kesi za jinai na madai, yanayohusu kesi za udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Alisema kwa mujibu wa Takwimu kutoka Mtakwimu Mkuu wa serikali, matukio ya ukatili na Udhalilishaji 865 yameripotiwa Mahakamani, na malalamiko 200 ya Udhalilishaji yamepokelewa ZAFELA kwa mwaka 2021.
WASIMAMIZI TUNZO
Mwenyekiti wa Kamati ya Tunzo za vinara wanaopinga Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia mwaka 2022, ambae pia ni Mkufunzi Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA, tawi la Kilimani, Imane Duwe, alisema wameandaa tunzo kwa wanaharakati ili kushirikiana kutokomeza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar.
Aliwasihi wanaharakati waongeze juhudi kubwa za kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ambapo kwa mwaka 2022, ulijumuisha watu 40, huku watu 467 walipiga kura kwa washiriki 59 na kupata washindi 12, katika vipengele 12 vya tunzo mbali mbali.
Alifahamisha kuwa katika kuhakikisha wanamaliza tatizo hilo wanafanya juhudi mbali mbali kwa jamii ikiwemo kufanya ushindani wa wanaharakati juu ya kupinga vitendo vya Udhalilishaji wa kijinsia.
KITUO CHA HUDUMA ZA SHERIA
Mwanaharakati kutoka Kituo Cha Msaada wa huduma za Kisheria, Fatma Khamis, aliwashauri wanaharakati wa kupinga Udhalilishaji wa kijinsia kujitoa kweli na kuhamasisha wengine kufanya shughuli hiyo ili kufikia malengo.
Alieleza kuwa na ari ya kupambania haki za wanawake na watoto kuhakikisha kundi hilo linakuwa salama katika mazingira yote anayoishi.
SHIRIKA LA LEGAL SERVICES FACILITIES (LSF)
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Lulu Mwanakilala alisema katika kuhakikisha wanawake na watoto wanapata haki zao, shirika lina tekeleza programu za ufikiaji wa haki kwa nchi nzima hususan wanawake na watoto, kundi hilo linapaswa kulindwa ili kufikia haki zao hata baada ya ndoa kuvunjika.
SHIRIKA LA WANAWAKE KATIKA SHERIA NA MAENDELEO BARANI AFRIKA (WILDAF)
Afisa wa Shirika la WILDAF, Vera Senga, alisema shirika linafanya kazi na wadau mbali mbali ili kutokomeza masuala ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto na ili wapatiwe haki zao kwa mujibu wa sheria zinazowalinda.
Akizungumza katika usiku wa kukabidhi tunzo kwa vinara 12 wa kupinga vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto, Disemba 3 mwaka huu Mwenyekiti wa Taasisi ya Maisha Bora Foundation, Mama Maryam Mwinyi alisema, wanaharakati bado wanakazi kubwa ya kuisaidia jamii kuondokana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, kwa kuitangaza tabia hiyo kuwa ni janga linalohitaji dharura na kuondokana nalo katika jamii.
Mama Maryam ambae ni Mke wa Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewasihi wanaharakati kusimama kidete katika kukemea na kuhakikisha sheria zilizotungwa zinatumika ipasavyo, kuepusha wanawake na watoto kudhalilika.
“Niwasihi wanaharakati kuendelea na moyo wa kujitolea katika kuinusuru nchi yetu na vitendo vya udhalilishaji kwa kuongeza bidii katika mapano hayo” alisema.
Aidha alieleza wazi kuwa Mapambano dhidi ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia ni suala nyeti, linahitji umakini mkubwa kutokomezwa, wadau kushikamana ili kuondoa tabia hiyo na kubaki historia.
Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wadau, wanaharakati, kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
WIZARA.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Abeda Rashid Abdallah, alisema wizara inapambana na vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na Watoto kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Alisema ni vyema kuondosha tabia ya kuwafanya wanawake hasa wajane ni watu wasiyo na haki ya kupewa mali, matunzo, kutokana na chuki zao binafsi kwani madhara yake ni makubwa.
Aibainisha kuwa Serikali imefanya juhudi mbali mbali kukomesha tabia ya kuwakosesha wanawake na watoto haki zao, ikiwemo kujenga Mahakama maalumu, na kuweka sheria madhubuti kwa watendaji wa kesi hizo.
Alieleza kuwa Wanawake na watoto wana nafasi kubwa ya kutumika taifa na kuleta maendeleo nchini jamii haipaswi kulibeza na kulinyima haki zake stahiki.
Alisema sheria zilizopo zinatoa muongozo wa kupatiwa haki zao wanawake, watoto na makundi mbali mbali, kila mmoja anapaswa kutekeleza haki ya mwenzake.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma, alisema udhalilishaji wa kijinsia ni janga la taifa jamii inapaswa kuungana kumaliza tatizo hilo kila mmoja kuwa sehemu ya mpambanaji.
Alisema katika kuhakikisha suala hilo linaondoka Zanzibar, kupitia siku 16 za kupinga ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia wizara ilitoa zawadi kwa watu wa makundi tofauti ili kushajihisha kupinga vitendo vya udhalilishaji.
Alisema bado vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia vina endelea kufanyika, wizara imefanikiwa kutoa zawadi kwa wananchi mbali mbali wanapinga vitendo hivyo ili kuhamasisha wengine kupambana.
Aliwahakikishia wanaharakati kuwa wizara ipo tayari kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi kutokomeza udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Alieleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 katika sura ya 8 kifungu 211, imeeleza kusimamia upatikanaji wa haki ya kulindwa dhidi ya ubaguzi, udhalilishwaji, dhuluma, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.
Aidha dira ya Zanzibar ya 2020 inatoa mfumo wa uchumi wa jumla na kubainisha mikakati ya maendeleo ya binadamu inayozingatia jinsia, ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa jinsia zote na kuondoa upendeleo wa kijinsia katika upatikanaji wa rasilimali, pamoja na kuimarishwa kwa ushiriki katika maamuzi na umiliki wa mali.