NA ASIA MWALIM
LICHA ya Serikali kuanzisha mradi wa kurejesha madarasani watoto walioacha skuli, bado kundi kubwa la watoto wapo mitaani wakizurura ovyo na wengine kutumia muda huo kufanya kazi, hali ambayo hudumaza maendeleo.
Ili Serikali kufikia adhma ya kurejesha skuli watoto Thelathini na tano elfu, (35,000) kwa kipindi cha miaka miaka 3, kila mmoja katika jamii, anapaswa kushiriki mradi huo kikamifu na sio kuachia wazazi wakike pekeyao, itasaidia kupata nchi ya wasomi.
Inaamika kuwa nchi isiyo na wasomi maendeleo yake huchelewa, kwa mantiki hiyo ni wajibu wa wazazi, walezi na jamii kiujumla kushirikiana na serikali kuwarejesha madarasani watoto walioacha skuli na sio kuachia mzigo huo wanawake kwa visingizo.
Penye nia pana njia, huu ni msemo maarufu unaotumika kwenye suala la kuleta manufaa, kama ilivyo Serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, imedhamiria kuimarisha sekta ya elimu kwa watoto wa rika zote.
Mradi wa kurejesha watoto skuli umeanzishwa mwaka 2021, unatarajiwa kumalizika 2023, unatekelezwa chini ya uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Kwa mujibu wa utafiti wa mapato na matumizi ya kaya kwa mika 10 iliyopita, kutoka Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, unaeleza kuwa watoto chini ya umri wa miaka 17 wanaathiriwa na matatizo mbali mbali ikiwemo elimu, afya, makaazi bora, lishe na maeneo mengine hali inayochangia kwa kiasi kikubwa watoto hao kuendelea kuwa maskini.
WAZAZI WA WANAFUNZI.
Mwajuma Khamis Haji, mzazi wa mwanafunzi, alieacha masomo darasa la sita, alisema kwa mara ya kwanza amegundua mtoto wake ameacha skuli baada ya kusikia kwa majirani wanaoishi pamoja, alipofatilia kwa undani tayari mtoto wake alianza kushiriki vijiwe.
Alisema kukosa elimu ya lazima kumefanya maisha ya mtoto wake yanazidi kuwa magumu siku hadi siku tangu kukatisha masomo kutokana na kufanya kazi zisizo rasmi ikiwemo ufugaji wa ng’ombe.
Kuelewa dhana ya mradi huo, amechukua jitihada za kumrejesha mtoto huyo skuli lakini hakufanikiwa kwa sababu hapati mashirikiano kwa mzazi mwenzake.
“Mume wangu suala la elimu hajalipa kipaumbele, ameshikilia mtoto wa kiume ana uwezo wa kufanya kazi yoyote” alisema mzazi huyo.
Mzazi huyo alisema sio sawa watoto kuacha masomo kwani athari kubwa atazipata katika maisha yake, aliomba serikali kuwa na sheria zitakazo wabana wanaowatumikisha watoto hata wazazi.
Patima Vuai Hassan, mzazi aliefanikiwa kumrejesha mtoto darasani, skuli ya Umbuji Wilaya ya Kusini Unguja, alisema wanafunzi wanatabia ya kuiga vitu kutoka kwa wengine ni vyema wazazi kurejesha malezi ya pamoja ili kuwajengea maisha mazuri watoto.
Alisema tangu mtoto wake kurudi skuli kupitia Mradi ulionzishwa anafanya vizuri, anasoma kwa bidii kutokana na kupatiwa sare za skuli ambapo awali alisoma bila ya sare.
Sababu kubwa inayowafanya watoto wa vijijini kutoroka skuli ni kuona watoto wengine wakifanya kazi, pia kijiji cha Umbuji hakina muamko katika kusoma.
Tangu mtoto wake amerudi darasani kwa mara nyengine mafanikio makubwa amepata kupitia darasa la elimu mbadala, ikiwemo ujuzi wa Komputa na shughuli za ujasiriamali.
Said Ussi Said alisema, mara nyengi wanaume wanabeba majukumu ya maisha kwenye familia ni vigumu kuwafatilia watoto mara kwa mara ingawa wanajua ni wajibu wao, aliwataka wanaume kupanga muda maalumu wa kuangalia familia na sio shughuli za maisha tu.
WANAFUNZI
Hamoud Muhammed Makame, mwanafunzi alieacha masomo alisema, alipokua darasani alijitahidi kusoma lakini walimu wake hakuwafahamu.
Alisema bora mwanafunzi apewe uhuru wa kuchagua masomo ya ujuzi mapema kwani anapendelea kutengeneza magari.
Aliongeza kuwa ameamua kufanya kazi kwa sababu anapenda kujituma ili kupata pesa za mahitaji yake ya sikukuu.
Khatibu Abdallah, mwanafunzi alierudi darasani alisema sababu kubwa iliyomkatisha masomo awali ni kukosa mahitaji ya chakula na mavazi kwani hana uhakika wa kupata huduma hizo.
Aidha alisema wakati alipokua mtaani hakuna faida aliyoipata badala yake amepoteza muda kucheza gemu, kuogelea, na mpira, pia anajutia suala hilo, kwa sasa anasoma kwa bidii anatarajia kuwa fundi wa umeme.
WALIMU WA SKULI
Wameeleza kufurahishwa na mradi huo na kuwataka wazazi, walezi kushirikiana kwa pamoja katika kukaa karibu na watoto hao ili kuwaongezea hamu ya kupenda kusoma.
Mwalimu Mkuu skuli ya Umbuji, Ramadhan Mrisho Juma alisema elimu ni haki ya kikatiba kwa wanafunzi wote ni vyema wizara kutoa nguvu ya ziada kwa kuwachukulia hatua haraka wazazi na watoto wanaoacha masomo kwa makusudi.
VIONGOZI WA SHEHIA
Sheha wa shehia ya Umbuji, Mohammed Mrisho Juma, alisema wazazi wa Umbuji hawana muamko wa elimu, mara nyingi hufanya shughuli za kilimo na ufugaji, aliomba serikali kutoa adhabu kwa mzazi au mlezi asietaka kuwajibika kwenye mradi huo.
wazazi wanajukumu kubwa la kuhakikisha watoto wanaohusika kujiunga na madarasa hayo wanaendelea na masomo ili kuwajenga uwezo wa kimaarifa.
MTANDAO WA HAKI ZA BINADAMU
Mkurugenzi wa Mtandao wa Haki za Binaadamu Tanzania, Onesmo Olengurumwa, alisema kwa mujibu wa sheria za kitaifa, kimataifa na mikataba ya haki za binadamu zinatambua kuwa elimu suala la la haki kila mmoja anapaswa kuzingatia.
Aidha alisema Mataifa yenye uchumi mkubwa kama Marekani yamepiga hatua baada ya kuwa na wasomi na wabunifu, jamii ya Tanzania haipaswi kupuuza suala la elimu haswa kwa watoto ambao ndio viongozi wa baadae.
SHIRIKA LA UNESCO
Mwakilishi wa Shirika linaloshughulikia Watoto Duniani (UNICEF) Shalini Buhuguna, alisema licha ya watoto wengi wanaishi na umasikini, lakini kupitia Mradi huo Zanzibar imepiga hatua katika mipango yake ya kupunguza umasikini kwa watoto.
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekua na sera ya kumjali mtoto ikiwemo ya kwarudisha skuli ili kupata elimu kwa maendeleo yake na taifa.
Alifahamisha kuwa mipango ya UNICEF ni kuendelea kushirikiana na Serikali ya Zanzibar katika mpango wa kuwajali watoto katika nyanja mbali mbali, ikiwemo kupatiwa elimu, na makuzi yao.
Kaimu Divishen wa Pato la Taifa Khalid Chum alisema, wakati huu wazazi walipaswa kuhakikisha watoto wao wanapata elimu na sio kuwatumikisha au kuwaacha wakifanya kazi, ili kupunguza kiwango cha umaskini nchini.
Aidha alisema serikali inatarajia watoto wote wawepo madarasani wakipata elimu na sio kufanyakazi zisizo rasmi kwani suala hilo huathiri maendeleo yao.
Alieleza juhudi zinazofanywa na serikali kwa watoto zimesaidia kupunguza umasikini kwa kipindi cha miaka 10 kwa asilimia 9.2, kutoka asilimia 34.9 mwaka 2009 hadi asilimia 30.4 kwa mwaka 2015, imepungua kutoka 25.7 hadi asilimia 9.2 kwa mwaka 2019.
Kuwatumikisha watoto chini ya umri wa miaka 17 wanaotakiwa kusoma tafiti inaonesha kunaleta changamoto ya umasikini kwa watoto hasa maeneo ya vijijini kwa Unguja na Pemba.
IDARA YA ELIMU MBADALA
Mratibu wa Mradi wa kurejesha watoto skuli, Mzee Shirazi Hassan, alisema moja kati ya mikakati waliofanya baadhi ya maeneo ni kufungia vituo vya kuchezea gemu wakati wa skuli, na kuelimisha shehia mbali mbalii, pia wanatarajia kuandaa sheria ndogo ndogo ili kuwatia hatiani wazee wasioshiriki kupeleka watoto skuli kwa makusudi.
Alisema lengo la mradi wa kuwarudisha darasani wanafunzi walioacha masomo na waliokosa fursa ya kusoma, utashirikisha wanafunzi wa miaka 7 hadi14, kusoma darasa la mbadala, na kuanzia miaka 15 kupatiwa mafunzo ya amali.
Aidha alisema wanafunzi hao husaidiwa vifaa vya kujifunzia kama vile madaftari, vifaa vya kuandikia na kuchorea, sare, mabegi ili kuyafanya madarasa hayo kuvuti wanafunzi ili wapende kusoma na kubaki darasani.
Alisema miradi huo wa miaka mitatu umefanikiwa kurejsha watoto elfu 10, ambapo wanatarajia kupata wanafunzi elfu 35, kwa mikoa yote ya Zanzibar.
Alieleza kuwa wanafunzi 3,033 wakiume na wanafunzi 2,517 wakike wamerudishwa madarasani kwa upande Unguja.
Pia wanafunzi 2,934 wakiume na 1,697 wanawake kwa upande wa Pemba.
Alisema Takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Kaskazini A Unguja unaongoza kurejesha wanafunzi 1,287 na Mkoa wa Micheweni Pemba unaongoza kurudisha idadi ya wanafunzi 2,033.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima, Mashavu Abdallah Faki, alisema wamefanikiwa kupata wanafunzi elfu 10, kutokana na juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na serikali, wadau pamoja na walimu.
Aidha alisema, Idara itasimamia mikakati yake kwa mujibu wa sheria zinazomlinda mtoto kupata haki ya elimu, hivyo mzazi yoyote atakaeshindwa kutoa mashirikiano atahusika kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
WIZARA YA ELIMU
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Abdul-gulam Hussein, alisema kufanikiwa mradi huo utaifanya Zanzibar itambulike kuwa nchi ya mwanzo kufanya vizuri duniani, na kupata watoto wenye maisha mazuri ya baadae.
Alisema wizara imekuwa ikiandaa progamu mbali mbali kuona kila mtoto anapata elimu kutokana na mahitaji yake, ikiwemo kuanzishwa kwa madarasa ya elimu mbadala ili kuhakikisha watoto wa rika zote wanapata elimu, maarifa na ujuzi, wa kuwawezesha kufanya ushindani wa soko la ajira na kuwa viongozi bora wa baadae.
Akizungumzia kuhusu kuchukuliwa hatua wanaotumikisha watoto alisema sheria zilizopo zinapinga suala hilo na wizara inafatilia kwa karibu kuona namna ya kumaliza tatizo hilo.
Alisema katika kuhakikisha mradi huo unafanikiwa kwa kiwango kikubwa serikali ilitoa maagizo kwa viongozi mbali mbali wa mikoa, wilaya na shehia kufatilia watoto walioacha skuli waweze kurejeshwa na zoezi hilo linaendelea.
Alieleza kuwa, Chama Cha Mapinduzi(CCM) kinaamini kuwa elimu bora ndio nyenzo muhimu ya kujenga, kulea na kuendeleza rasilimali watu ili kuchangia kikamilifu ujenzi wa Taifa na maendeleo ya jamii.
SHERIA YA ZANZIBAR
Sheria ya Zanzibar inaeleza kuwa kila mzanzibari ana haki ya kupata elimu. Katiba ya Zanzibar 1984 sura ya 2 kifungu cha 10 (d) inazungumzia kuwa elimu ni moja ya haki za binadamu linapaswa kuzingatiwa.
DIRA ya mpango wa maendeleo kwa mwaka 2050 inaeleza mikakati yake ya mfumo wa elimu ni kuhakikisha inatoa elimu bora, mafunzo ya kujipatia kipato ili kumnyanyua kiuchumi.
Mapatano ya kimataifa juu ya Haki za Watoto yamekubaliwa na wanachama wa Umoja wa Mataifa, kuwa watoto wanahaki ya kupata mahitaji ya elimu.
Katika Ibara ya 26 ya tamko la haki za binadamu imesisitizwa haki ya kila mtu kupata elimu, na kusoma kadri apendavyo bila kujali kabila, rangi au uraia, na kuitaka serikali kutekeleza haki ya elimu kwa wote.
Mradi wa kuwarejesha watoto skuli unatekelezwa na wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar kwa ufadhili wa shirika la UNICEF pamoja na taasisi inayoshughulikiaaaaaaa masuala ya elimu kwa wote EAC kutoka QATAR.