Uislamu unasisitiza umoja, mshikamano

KUR’AN tukufu inatutaka waislamu tuwe wamoja na inatukataza tusifarikiane, kama ilivyoeleza, “Na kwa yakini huu umma wenu ni umma mmoja na mimi ni Mola wenu mlezi, basi nicheni mimi”. Al-Muminuun (23:52).

Ushahidi mwengine unaowaelekeza waumini wasifarikiane unaobainishwa katika surah Al Imraan (3:103), “Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane”.

Waislamu tuna dini inayosisitiza umoja, tofauti na hali halisi tuliyonayo ambapo tupo katika msambaratiko mkubwa, ingawa ni kweli uislam ni dini isiyoeleweka vyema miongoni mwa wasiokuwa waislamu, pia uislamu ni dini isiyoeleweka vyema miongoni mwa waislam wenyewe.

Chanzo kikuu cha mifarakano ndani ya waislam na kukosa maendeleo ya pamoja ni kutofahamu vyema uislam wenyewe, waislamu wamekuwa wepesi kuitana makafiri wakati uislamu unataka tushikamane na nembo ya uislamu.

Waislamu tunashindwa kuheshimiana na kuvumiliana kwenye ibada kwa misingi ya madhehebu, wakati kuwepo kwa ibada ya hijja sote husali nyuma ya imamu mmoja kungetosha kuwa ni somo la kuzingatia la umoja na uvumilivu baina yetu.

 

UKONGWE WA IKHTILAAF

Kwa mujibu wa kur’an, tofauti (ikhtilaaf) zimeanza tangu katika maumbile kuanzia miti, milima, wadudu, wanyama mpaka binadamu.

Na inaeleza pia kuwa binadamu tumetofautiana hata katika rangi, lugha, lafdhi, lahaja na kadhalika.

Utofauti huo katika uumbaji ni alama ya uwepo wa Mwenyezi Mungu na pia ni kuonesha weledi na umahiri wake wa pekee katika uumbaji. Busara ni kuzitumia tofauti hizo kama msingi wa nguvu na sio udhaifu.

Ikhtilaaf katika dini nazo zilianza zamani ambapo hata manabii walikuwa na tofauti zao. Nabii Musa AS alitofautiana na nduguye Nabii Haroun (AS) katika ufahamu na kuyapima mambo. Nabii Suleiman (AS) na Nabii Daud (AS), ambao ni mtu na mwanawe walitofautiana katika hukumu ya kesi ya mkulima na mfugaji.

Lakini pia kulikuwa na ikhtilaaf miongoni mwa masahaba kwenye uchambuzi wa mambo katika matukio na mazingira tofauti. Na Masahaba wa Mtume (SAW), walipishana katika ufahamu na rai wakati Mtume (SAW) yuko pamoja nao.

Hadithi iliyopokelewa na Ibn Umar RA kuwa siku ya Al-Ahzaab, Mtume (SAW), aliwaambia masahaba kuwa, asisali mmoja wenu sala ya Laasiri isipokuwa asali mahali panapoitwa Banu Quraidha.

Sala ya laasiri ikawa inaingia na bado wakiwa njiani hawajafika eneo la Banu Quraidha. Kukagawika makundi mawili: kundi moja walisema, hatutosali Laasiri mpaka tufike Banu Quraidha kama alivyoagiza Mtume (SAW) kwani hatupaswi kukhalif amri yake.

Na kundi jengine wakasema, hapana, tutasali mahali hapa hapa kwani wakti wa sala umewadia na Mtume (SAW) haendi kinyume na maagizo ya kur’an yanayotaka sala isaliwe kwa wakati.

Pakazuka ikhtilaaf miongoni mwa Masahaba za ufahamu na rai ambapo kundi moja halikusali pale kwa kuchukua maana ya nje (dhahir ya maneno) ya amri ile ya Mtume SAW, na kundi jengine likasali pale kwa kuchukua manaa ya ndani (jawhar ya maneno) ya amri ile ile ya Mtume (SAW).

Baadaye tukio lile liliposimuliwa mbele ya Mtume (SAW) hakukemea kundi lo lote kati ya yale mawili bali alithibitisha kwamba makundi yote yalifanya vizuri na sahihi na kwa hivyo yote yalipatia na kusibu.

Moja ya somo la kuzingatia katika tukio hili ni kuwa Mtume (SAW) aliuacha mlango wa ijtihaad wazi kwa ajili ya watu kutofautiana kimtazamo kwa dalili na hoja.

Angeweza kusema kuwa kundi moja liko sahihi na moja limekosea, lakini hakufanya hivyo, na badala yake aliwacha mlango wazi katika ufahamu ilimradi kuongozwe na juhudi zinazosimama juu ya ikhlasi, unyenyekevu na namna iliyo bora na halali.

Na tukio hili linathibitisha kwamba masuala ya dini hasa upande wa fiqh hayakomei kwenye rai moja tu, bali yanakubali uwepo wa tofauti katika mitazamo na ufahamu na kwamba maoni tofauti yanaweza kuwa sahihi kwa wakati mmoja.

Kama hivyo ndivyo, itakuwa SI sahihi kumuita Muislam kafiri kwa sababu anapinga Maulidi, Khitma, Talaqini au anafuata muandamo wa kimataifa na kadhalika. Sambamba, itakuwa si sahihi pia kumuita Muislam kafiri kwa sababu anayaunga mkono maulidi, hitma, talaqini au anafuata muandamo wa kitaifa na kadhalika.

Tuache kuweka mbele tofauti za madhehebu kwa kuugharimu Uislam kwani Uislam ndio utambulisho wetu wa kwanza tuliopewa na Nabii Ibrahim AS. “Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim. Yeye alikuiteni waislamu tangu zamani na katika hii (kur’ani) pia.”

Ibadhi asingekuwa ibadhi ila alikuwa kwanza muislam. Sunni asingekuwa sunni kama kwanza hakuwa muislam ndio akawa sunni. Shia asingekuwa shia kama hakuwa kwanza muislam halafu ndio akawa shia. Vivyo hivyo kwa suffi, salafi, answaru sunnah, tariqa nakadhalika.

 

HALI HALISI

Umezuka utamaduni ulioshtadi wa majibizano yaliyokosa ustaarabu wa majadiliano baina ya masheikh hasa kupitia mitandao ya kijamii ambayo sio afya kwa uislam.

Mtindo huu unatuyumbisha wafuasi katika kufahamu masuala ya Dini yetu na wakati mwengine hata kupandikiza chuki, uhasama na uadui baina yetu.

Masheikh kila wakikaa pamoja katika maelewano, wakaheshimiana na kuvumiliana katika tofauti zao za mitazamo ndio jambo bora zaidi katika maendeleo ya dini yetu katika dunia hii na kesho akhera.

Vyenginevyo, hatutaweza kuwa na harakati za Kiislamu zitakazoweza kuleta maendeleo katika nyanja yo yote kama tutaendelea kubakia na mifarakano ya aina hii.

 

JAMBO LISILOPINGIKA

Ikhtilaaf haziwezi kuondoka kwa vile tunafikiri tofauti. Mwenyezi Mngu SW Ametuumba tofauti na kwa sababu hio bila ya shaka yo yote tutatofautiana katika ufahamu, rai, uchambuzi, maono na mitazamo.

Na kwa hakika, ukiona watu wawili wanakubaliana juu ya kila jambo, basi elewa kuwa mmoja wao hafikiri maana kimaumbile hatuwezi sote kuwa sawa katika kufikiri na ufahamu hata kama sote tutakitazama kitu hicho hicho kimoja.

Ndio maana watu tofauti walio na rasilimali sawa katika hali ile ile wakipewa nafasi na fursa sawa watatoa matokeo tofauti. Huo ndio uhalisia wa maumbile.

 

Ushauri

Waislamu wa Madhehebu yote na wa Makundi yote tunapaswa kuishi kwa pamoja chini ya vazi la Uislamu katika ufahamu wake, uvumilivu, na ukarimu wake kwani umoja na mshikamano ni muhimu kwa waislamu wa madhehebu yote kama ambavyo Qur’an (21:92) imetangaza kuwa Waislamu ni Umma Mmoja (Ummatan Waahidatan).

Hivyo, kwa pamoja tusaidiane kuzitumia tofauti zetu kwa mtazamo chanya wa kuzalisha anuai za rai kwani umma unakabiliwa na masaibu makubwa na Makundi yetu yote/madhehebu yetu yote yanalengwa na adui mmoja.

Vipengele vya kuimarisha umoja vinapaswa kutawala na mizozo kuepukwa. Na ikiwa jambo linaonekanwa linaleta mizozo, mifarakano na kukatana mapande baina ya waislamu ambalo bila ya shaka ni uovu mkubwa.

Ni vyema kuliwacha na kulinyamazia kwani hekima zinatueleza kwamba, ikiwa uovu tunaotaka kuuondoa (kama ni uovu) kwa kuundoa kwake utazuka uovu mwengine mkubwa zaidi kuliko huo tuliotaka kuuondoa basi busara ni kutokuondoa.

Aidha, ni muhimu kwa viongozi wa madhehebu na wa makundi kuzingatia mambo ya makubaliano, na si yale ya tofauti baina yao hasa kwa kuwa mambo ya makubaliano ndio yanahusu masuala ya msingi ya dini (usuul/shina) wakati mambo ya tofauti yanakhusiana zaidi na yale mambo madogo (furuu/matawi).

Madhehebu na makundi yote yanaamini juu ya nguzo sita za imani kuanzia uwepo wa Mwenyezi Mungu (SW), juu ya siku ya hukumu, kuhusu Mtume Muhammad (SAW) kuwa ni wa mwisho na yote aliyokuja nayo, kuhusu Mitume wengine, kuhusu vitabu vyote vya mbinguni, kuhusu malaika na qadar.

Vile Vile, madhehebu yote yanakubali kwamba waislamu wanapaswa kuzingatia nguzo tano za uislamu, yaani, kushuhudia kwamba hakuna Mola wa haki na anaepaswa kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu mmoja asie na mshirika na kwamba Muhammad (SAW) ni Mtume wake, kutekeleza na kusimamisha sala tano, kutoa zaka, kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuhiji Makka.

Kama hivyo ndivyo, waislamu tuungane na tufanye kazi pamoja katika yale ambayo sote tunaafikiana na tuheshimiane na kuvumiliana katika yale ambayo kila mmoja ana rai yake; tutizame matokeo yake itakuwa nini kama sio mafanikio makubwa kwa umma wenyewe wa Kiislamu na maendeleo yake, kwa ulimwengu na hata kuiongoza tena dunia. Wala utofauti wa mambo kati yetu si kasoro.

Kutokukubali kuwa tuko tofauti ndio kasoro yenyewe. Mkono hutusaidia katika kazi; lakini vidole vya mkono havilingani; hata hivyo; vyote hufanya kazi kwa pamoja.

Kasoro ya ufupi au urefu wa kidole hauondoi umuhimu wa kuwa sehemu ya mkono. Hivyo, tusitafute usawa wa fikra au mitazamo. Tukubaliane tupo tofauti kwa faida ya wote na kwa afya na maslaha ya Uislamu.

Mfano wetu Waislamu uwe ni mfano wa mwili mmoja kama alivyosema Bwana Mtume SAW na kwamba ukipata malalamiko ya kuumwa kiungo kimoja tu, basi mwili wote ushiriki katika hayo maumivu.

Jino likiuma mathalan, basi utakosa usingizi na viungo vyote vitasumbuka na vitashiriki kulalamika katika msononeko wa kuumwa kwa jino na kukesha pamoja. Waislamu kwa umoja na pamoja tushirikiane kuirudisha taswira hii aliyotuwekea Mtume SAW ya kuwa mwili mmoja maana hivyo ndivyo tunavyostahili kuwa.

 

HITIMISHO

Ikiwa kur’an (3:64), imetutaka waislamu kujadiliana na Ahlul Kitaab (mayahudi na Manasara) tena kwa njia iliyo bora, inakuwaje waislamu wenye kur’an hiyo hatuwezi kufikia ufahamu huo na maelewano kati yetu wakati mambo yanayotuunganisha pamoja waislamu ni muhimu na makubwa zaidi kuliko yale yanayotutofautisha?

Umma mkubwa kama huu wa waislamu unaotengeza sehemu kubwa ya waumini wa dini duniani wapatao bilioni 1.8 ukisambaratika kwa kuweka mbele mifarakano kuliko mambo muhimu yanayotuunganisha itakuwa ni hasara kubwa.

Binafsi sifungamani na dhehebu lolote najihusisha kuyasoma, kuyaheshimu na kuchagua mambo mema zaidi ya kujihusisha nayo kutoka kila dhehebu, na huu ni muongozo wa kur’ani: “Basi wabashirie waja wangu. Ambao husikiliza maneno, wakafuata yaliyo bora zaidi. Hao ndio Aliowaongoa Mwenyezi Mungu na hao ndio wenye akili.” Surah Azzumar.

Nathamini sana ubora wa kazi kubwa, ngumu, nzuri na muhimu walioifanya maimamu wa madhehebu yote juu ya uhuru wao wa mawazo na kuishi kwao pamoja kwa maelewano na kuvumiliana.

Kwa kheri na baraka za mwezi wa kheri na baraka, mwezi mtukufu wa Ramadhani, tunamuomba Mwenyezi Mungu (SW) awalipe maimamu na wanazuoni wa madhehebu na wa makundi yote malipo mema na makubwa kwa nia.

Ikhlas na juhudi za kazi adhimu walizofanya ikiwa ni pamoja na kutuachia historia ndefu na ya maana sana yenye utajiri mkubwa wa ilimu na urithi mpana wa maono na maarifa ulionufaisha maisha ya mamilioni ya Waislamu na wengineo kwa karne nyingi.

 

Khaleed Said Suleiman

+1 266 577 4303

Khaleed_ihaab@yahoo.com