NA JOSEPH NGILISHO, MANYARA
ASKARI wa jeshi la polisi mkoani Arusha, F3544, Sajenti Ismail Rashid Katenya (49), amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kutiwa hatiani na mahakama kuu kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi.
Hukumu hiyo ilisomwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara, John Kahyoza, katika wilaya ya Babati.
Katika hukumu hiyo, Jaji Kahyoza alisema mshtakiwa alikiuka kifungu cha 15 (1)(a), (3)(iii) cha sheria ya mwaka 2019 ya kudhibiti dawa za kulevya, sura ya 95 kama ilivyofanyiwa marejeo.
Kwa mujibu wa Jaji huyo, mshtakiwa pia alikiuka kifungu cha 18 cha sheria namba 5 ya mwaka 2001, ikisomwa pamoja na aya ya 23 ya nyongeza ya kwanza ya sheria ya uhujumu uchumi.
Mshtakiwa alikamatwa Januari 22, 2024 katika kijiji cha Silaloda, kilichopo wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara akisafirisha bunda 380 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 160.9, akitumia gari yake aina ya Nissan Patrol yenye namba za usajili T 148 CTB.
Awali, Wakili wa serikali, Rose Kayumbo, akisaidiana na Mawakili Wandamizi, Roberth Kidando, Edith Msenga na Leonce Bizimana, aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu ya kifungo cha maisha kwa kuwa kosa hilo lina adhabu moja tu.
Aidha, wakili huyo aliiomba mahakama pia itoe amri ya kutaifisha gari lake ambalo lilitumika kusafirisha dawa hizo, ili liwe mali ya serikali.
Hata hivyo, wakili mkuu wa utetezi, Fides Mwenda, aliiomba mahakama imuonee huruma na kumpa adhabu ndogo kwa kuwa ni mkosa wa mara ya kwanza, ni mtu mzima na ana wategemezi.
Akitoa utetezi wake, mshtakiwa aliieleza mahakama kuwa alienda shambani kwake Mbulu akiwa amebeba mbegu za vitunguu saumu, lakini baada ya kugongana na gari la polisi, walimbambikizia dawa hizo.
Baada ya utetezi huo, Jaji Kahyoza alimtia hatiani na kumpa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, huku akiamuru gari lake litaifishwe endapo ndani ya siku 60 hakuna mtu yeyote atakayejitokeza kudai kuwa ni mali yake.