MABOMU ya kutoa machozi au vitoa machozi ni mkusanyiko wa kemikali ambazo hukera neva na tezi za macho na kuanza kutoa machozi.
Kwa kawaida kemikali zilizomo kwenye mabom hayo husababisha macho, pua na koo kuwasha na wakati mwengine kuvimba.
Mabomu ya kutoa machozi kwa kawaida hutumika yakiwa kwenye kopo ambalo hurushwa na kusababisha ukungu au vumbi jembamba hewani.

Wakati mtu anavuta pumzi, kemikali hiyo husababisha hisia inayowasha machoni na kwenye koo na kusababisha kuwa vigumu kupumua.
Mabomu ya kutoa machozi ni silaha inayotumiwa na polisi katika maeneo mbalimbali, ambapo mara hutumiwa kwenye umati kwa ajili ya kuvunja maandamano au kutuliza ghasia.
Licha ya kuitwa bomu la kutoa machozi, lakini sio kwamba ni bomu halisia, bali ni poda iliyoshinikizwa ambayo hutengeneza ukungu pale inaporushwa.
Bomu la kutoa machozi liligundulika kwa mara ya kwanza na wanasayansi wa Marekani mnamo mwaka 1928.
Kuna aina tatu pekee za mabomu ya kutoa machozi yenye uwezo wa kutumiwa moja chloroacetophenone (CN), la pili chlorobenzylidene malononitrile (CS) na la tatu Dibenz[b,f]-1,4-oxazepine (CR).
1-chloroacetophenone (CN)
Aina hii ya bomu la kutoa machozi husababisha uwasho wa macho, koo na ngozi, punde mwanadamu anapovuta pumzi huhisi macho kana kwamba yanachomwa.
Bomu hili husababisha kuona vizuri, kuna uwezekano wa kupoteza kuona, kuwashwa na kuungua pua, koo na ngozi, kuhisi maumivu kifuani na kusababisha ugumu wa kupumua.
Majaribio ya kemikali hiyo kali kwa wanyama kama panya, sungura na nguruwe yameonyesha kuwa na sumu kali hasa ikiingia mdomoni.
2-chlorobenzylidene malononitrile (CS)
Kemikali hiyo ilianza kutumika kudhibiti umati mapema miaka ya 1950, lakini hadi katikati ya miaka ya 1960 ndipo ilipoanza kutumika katika nchi kadhaa.
Nchini Uingereza kumekuwa na wasiwasi unaoendelea kuhusu matumizi ya gesi ya CS huku mamlaka ya polisi ikilaumiwa kwa matumizi ya kemimali hiyo.
Jicho ndio kiungo nyeti zaidi wakati wa kudhibiti ghasia kwa kutumia kitoa machozi kwa sababu hufanya macho kutoka machozi mengi, yanafumba na kufumbua pamoja na mienendo mingine.
Pia husababisha kikohozi, kuongezeka kwa kamasi, maumivu makali ya kichwa, kizunguzungu, kubanwa kwa kifua, kupumua kwa shida, athiri ya ngozi na kuwa na mate mengi mdomoni.
Dibenz[b,f]-1,4-oxazepine (CR)
Utafiti uliofanywa dhidi yakemikali hii, umebaini kuwa ni sumu yenye athari pale binaadam anapovuta kuingia machoni ama kooni mwake.
Uchunguzi katika mamalia mbalimbali umeonyesha CR kuwa na sumu kidogo ikilinganishwa na kemikali zingine zinazotumiwa kudhibiti ghasia kama vile gesi ya CS.
Hata hivyo iwapo itakupata kwa kiwango cha juu hali yako inaweza kuwa mbaya. CR ni kemikali inayokera macho na kusababisha kutoa machozi.
Maji ya pilipili
Kuna maji ya pilipili ambayo ni tofauti na mabomu ya kutoa machozi ya CN, CS na CR.
Kemikali hiyo yenye pilipili hutengenezwa kutokana na capsaicin, kiungo muhimu kwenye utengenezaji wa pilipili kali.
Maji ya pilipili hukera macho na kusababisha hisia za kuchomwa na maumivu pamoja na kutoona kwa muda.
Upofu huu wa muda huruhusu maofisa kuwazuia watu kuendelea kusababisha ghasia.
Pia husababisha kukera wa muda na kuungua kwa mapafu na kupelekea matatizo ya kupumua.
Mabomu ya kutoa machozi hufanya kazi vipi?
Mabomu ya kutoa machozi husababisha dalili mbalimbali za mwili kuchochea vipokezi vya maumivu.
Mara nyingi mtu anapojikuta kwenye mazingira yenye mabomu ya kutoa machozi, macho huwaka moto na kutoa machozi, kukohoa, kupiga chafya na kupumua kwa shida.
Vilevile, kemikali hiyo inaweza kufanya ngozi kuwasha na hata kutapika.
Lengo la utumiaji wa mabomu ya kutoa machozi ni kusababisha usumbufu na maumivu makali, hivyo kufanya iwe vigumu kwa watu kukaa katika eneo ambalo kemikali hiyo imetumiwa.
Namna ya kukabiliana na mabomu ya kutoa machozi
Wakati unapojikuta umerushiwa mabomu ya kutoa machozi bila shaka utakuwa unapitia madhara ya kemikali hiyo, lakini unaweza kufanya yafatayo kupunguza nguvu ya athari yake.
Songea sehemu yenye hewa safi haraka iwezekanavyo, kosha uso wako kwa kutumia maji ya baridi, pia unaweza kutumia mchanganyiko wa saline.
Mabomu ya kutoa machozi yanaweza kushika kwenye nguo, kwa hiyo, pindi unapofika nyumbani, toa nguo ulizokuwa umevaa na kuzifua peke yake.
Aidha, kuna wale ambao wanasema kuosha uso kwa maziwa na maji inaweza kusaidia kupunguza hisia za kuuungua.
Hata hivyo, unashauriwa kunywa maji mengi kusaidia kuondoa chembe zozote za mabomu ya kutoa machozi zilizosalia kwenye mfumo wa mwili wako.
Ikiwa dalili zako ni kali au una shida ya kupumua, ni vyema kutafuta matibabu hospitali.
Kwa ujumla athari za mabomu ya kutoa machozi zinaweza kutofautiana kulingana na umri, afya ya mtu na ikiwa pengine tayari ana maradhi mengine au yuko katika hatari ya kupatwa na magonjwa.
Athari ya muda mrefu ya mabomu ya kutoa machozi inaweza kusababisha matatizo makubwa zaidi kiafya, kama vile kuungua kwa kemikali kwenye ngozi na macho, upofu wa kudumu na uharibifu wa mapafu. Katika matukio nadra, imeweza kuhusishwa na kifo.