Skip to content

Chuo cha mipango chatakiwa kujikita kufanya tafiti

NA SAIDA ISSA, DODOMA 

NAIBU Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, amewataka wataalamu wa Chuo cha Mipango na Maendeleo vijijini Dodoma (IRDP), kufanya tafiti kwa lengo la kuongeza thamani ya madini na mazao ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na serikali kwa ujumla.

Alimuomba Mwenyekiti wa Baraza la uongozi wa chuo hicho, Profesa. Joseph Kuzilwa kupanua wigo wa kuongoza nguvu kwenye tafiti huku akisema zipo fursa kwa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Aliyasema hayo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa baraza la 13 la uongozi la chuo hicho.

Aliongeza kuwa serikali inahitaji tafiti zikiwamo ukusanuaji kodi, upatikanaji mapato ambazo zitasaidia kuongeza mapato yake.

“Nchi ina madini mengi na mafuta kwa mujibu wa wataalamu, tunaomba tafiti za namna ya upatikanaji wa madini na matumizi yake ili kuyaongezea thamani na kuachana na kuuza malighafi,”alisema.
Alisema anatambua wengi wao wana uzoefu wa kutosha wa kuongoza taasisi kupitia mabaraza, bodi za taasisi lakini bado katika ana wajibu wa kuwakumbusha majukumu yao kwa kuwa ndio utaratibu wao.

Alisema ni matumaini yake kuwa wataongeza mfumo wa kufundishia na kujifunza huku akisisitiza matumizi ya TEHAMA na kuimarisha huduma za kitaaluma.

Mkuu wa chuo, Prof. Hozen Mayaya, alisema mipango ya baadae ya chuo hicho ni kuendeIea na ujenzi wa miundombinu katika kampasi zote mbili, ambazo ni Dodoma na kituo cha mafunzo ya kanda ya ziwa Mwanza.

Aliongeza kuwa kipaumbele ni kumbi za mihadhara na dakhalia ili kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la makazi kwa wanafunzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa chuo hicho, Prof. Joseph, alisema wamepokea kijiti kutoka uongozi wa baraza walilomaliza muda wake ambalo lilifanya mambo mazuri na kwamba chuo hicho kwa sasa kina walimu wengi katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi wanoseomea kozi za uzamivu.