WANACHAMA wa kikundi cha kuweka na kukopa cha hifadhi (COCOBA) ha kijiji cha Chekereni Mikumi mkoani Morogoro wamepongezwa kwa kutumia vyema shilingi milioni 28.8 walizopatiwa kupitia mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii , Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mnzava alieleza kufurahishwa na maendeleo ya kikundi hicho kinachojishughulisha na uchakataji wa alizeti kuzalisha mafuta ya kupikia huku akiwataka kuendelea kujiimarisha zaidi.
Mnzava alieleza kuwa mradi huo pamoja na shughui nyengine unalenga kuimarisha maisha ya wananchi wanaoichi jirani na hifadhi kupata shughuli mbadala za kuwaingizia kipato badala ya kutegemea hifadhi hizo jambo linalodhoofisha juhudi za uhifadhi na utalii kwa ujumla.
Hivyo mwenyekiti huyo aliwahimiza wanakikundi hao kujishughulisha na shughuli za uhifadhi endelevu huku wakiwa mstari mbele kupinga vitendo vya ujangili wa wanyamapori na hujuma dhidi ya maeneo ya hifadhi.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii , Balozi Dk. Pindi Chana, mbali ya kuwapongeza wanakikundi hicho aliwataka kutumia fedha walizopewa na serikali kwa matumizi yaliyokusudiwa ili kukuza vipato na uchumi wao na familia zao.
Aidha Balozi Dk. Chana alieleza kuwa wizara yake inatekeleza mradi huo katika hifadhi mbali mbali kwa kuimarisha miundombinu, ujenzi wa majengo ya utawala na kupumzikia wageni lakini pia kuziwezesha jamii zinazoishi jirani na hifadhi ili zishiriki katika ulinzi na uendelezaji wa wanyama na maeneo ya hifadhi.
Awali akiwasilisha taarifa kwa kamati, Mwenyekiti wa COCOBA Chekereni, Rehema Njovu, alieleza kuwa kupitia mradi REGROW walipokea shilingi milioni 28.8 zilizotumika kwa kazi mbali mbali ikiwemo ujenzi wa jengo, kununulia mashine ya kukamulia alizeti na kuandaa shamba.
Alifafanua kuwa kupitia fedha hizo wanachama wa kikundi walifanikiwa kupata mikopo yenye riba nafuu iliyowawezesha kumudu gharama za maisha, kusomesha watoto na kupata faida itokanayo na mashine ya kuchakata alizeti kuzalisha mafuta ya kupikia.
Aidha Mwenyekiti huyo kupitia ziara hiyo iliyowashirikisha Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi, Watendaji na Maafisa Waandamizi wa wizara na hifadhi ya taifa Mikumi, aliishukuru wizara na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuvijali vikundi vya kijamii na kuvijengea uwezo ili vijikwamua kiuchumi.