KINSHASA, DRC
MAMLAKA nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimewaachia huru wafungwa wapatao 600 kutoka gereza kuu la nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka taifa hilo, kuachiliwa kwa wafungwa hao ni sehemu ya mchakato unaolenga kupunguza msongamano mkubwa wa wafungwa kwenye magereza ya nchi hiyo.
Waziri wa sheria wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Constant Mutamba alitangaza kuachiliwa kwa idadi hiyo ya wagungwa kwenye hafla iliyofanyika katika Gereza kuu la Makala liliopo mjini Kinshasa.
Mutamba alisema serikali ina mipango ya kujenga gereza jipya mjini Kinshasa, hata hivyo, waziri huyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu ujenzi wa gereza hilo jipya.
Kwa mujibu wa ripiti iliyotolewa hivi karibuni na shirika la kimataifa la Amnesty International, gereza la Makala ambalo ndio kubwa zaidi nchini humo lina uwezo wa kuchukua wafungwa 1,500, lakini linawahifadhi zaidi ya wafungwa 12,000 wengi wao wakisubiri kesi.
Mapema mwezi huu, kulitokea jaribio la kuvunja gereza ambapo watu 129 walikufa, wakiwemo wale waliopigwa risasi na walinzi na wengine kufariki katika mkanyagano.
Mkasa huyo ulitokea alfajiri ambapo milio ya silaha za kawaida na silaha nzito nzito ilisikika kwenye gereza hilo pamoja na viunga vyake, pale baadhi ya wafungwa walipojaribu kutaka kutoroka.
Pia kulikuwa na visa kadhaa vya wanawake kubakwa wakati wa jaribio hilo lakutoroka jela, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Congo Jacquemin Shabani alichapisha kwenye X mapema mwezi huu, bila kufafanua.