NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, amewaomba watanzania kupendana, kustamiliana na kuvumiliana ili kuijenga nchi kwa pamoja
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya amani duniani kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, alisema Tanzania ina watu zaidi ya milioni 60, hivyo haiwezekani kuwa na mawazo yanayofanana.
Alisema licha ya Tanzania kuwa na makabila mengi, dini tofauti na watu wenye vipato visivyolingana, tofauti hizo hazijawahi kutumika kuondoa amani ya nchi kwa sababu ya wanchi kuishi kwa kuvumiliana, kustahimiliana na kuridhiana.
“Utanzania wetu ni wa muhimu na hivyo tuungalie na tuulee kwani ni mti mkubwa na ikitokea mtu ana ukata asifikiri anakata kwa hasara ya mwingine bali amani ikitoweka tutaumia wote”, alitahadharisha.
Alisema katika nchi moja kuna watu wamepewa kipato cha kati,chini na matajiri lakini bado haliyawahi kuwa tatizo badala yake Watanzania wanaishi kwa amani huku akisisitiza licha ya tofauti nyingi zilizopo kamwe zisiwe sababu ya kugawanyika na kutafutana ubaya miongoni mwao.
Hata hivyo, alitahadharisha kwamba kama dini zitageuka kujadili dini ya wingine, mtu mwengine atapata nafasi ya kujadili dini ya mwezake na kwa vyevyote vile hakutakuwa na utulivu wala amani.
“Vilevile kama chama kimoja cha siasa kitajiita ni kikubwa na vyama vingine vidogo, chama kitafanya vyama vyengine kujiunga dhidi yake na matokeo yake amani itaondoka,” alisisitiza.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Sheikh Alhad Mussa Salum, alisema kupitia kongamano hilo viongozi wa dini wamefanya dua ya kuombea nchi na kutoa nasaha zao kwa kuwa nchi inapitia kipindi kigumu ikiwemo watu wasiojulikana.
“Hatuwajui sisi (watu wasiojulikana) lakini kwa Mwenyezi Mungu wanajulikana kwa hivyo kilichofanyika ni kumkabidhi Mwenyezi Mungu kwa sababu yeye anawajua, abadilishe nyoyo zao ili waache jambo hilo linalowatia hofu watanzania,”alisema.
Alisema kazi ya viongozi wa dini kuwaombea watu watendao maovu wabadilike, hivyo kupitia maombi yao Mwenyezi Mungu atawabadilisha.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisema Tanzania itaendelea kudumu katika amani, umoja na maendeleo kama wananchi wataendelea kupendana.