MWANAJUMA MMANGA NA NUSRA SHAABAN
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imetoa onyo kwa viongozi wa umma wanaowahamisha watumishi bila kufuata taratibu zilizoekwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Dk. Haroun Ali Suleiman, alitoa kauli hiyo, alipokuwa akijibu hoja za wajumbe wa Baraza hilo waliochangia bajeti kwa mwaka 2025-2026.
Waziri huyo alibainisha kuwa utaratibu wa kuwahamisha watumishi wa umma kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyengine serikalini umeekewa taratibu hivyo, viongozi lazima wazifuate taratibu hizo na sio kufanya wanavyotaka.
Alisema miongozo ya watumishi inapotolewa viongozi lazima waitekeleza, hivyo serikali haitosita kumchukulia hatua kiongozi yoyote atakayekiuka miongozo ya kiutumishi.
Dk. Haroun alisema serikali haitovumilia uhamisho wa watumishi usiozingatia sheria, kanuni na maslahi ya msingi ya watumishi, kwani jambo hilo linasababisha usumbufu na kushusha morali kazini.
“Watumishi wa umma wanapaswa kuheshimiwa na kuhamishwa kwa mujibu wa taratibu rasmi, si kwa matakwa binafsi ya viongozi”, alisema waziri huyo.
Dk. Haroun alisema serikali imeanza kuimarisha mifumo rasmi ya kiutumishi ili kuhakikisha maamuzi ya uhamisho yanafanyika kwa uwazi, uhalali na kwa mujibu wa sheria, hatua inayolenga kuondoa uonevu na maamuzi ya upendeleo.
Aliwahimiza maofisa utumishi kufanya kazi kwa uzalendo na uadilifu, wakizingatia misingi ya utawala bora badala ya kutumia nafasi zao vibaya kwa chuki, visasi au upendeleo.