NA MWAJUMA JUMA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema uwepo uwanja wenye viwango vya kimataifa umeiweka Zanzibar katika kiwango cha kimataifa kwenye ramani ya michezo.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana katika ufunguzi wa awamu ya pili ya New Amaan Complex kwa viwanja vya ndani vya michezo, maduka, maegesho mikahawa na hoteli ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kuadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema katika uongozi wake ameifanyia vizuri sekta ya michezo na wameacha alama, ambayo wataendelea kuiweka kwa maendeleo ya michezo nchini.
Hivyo alisema hakuna sababu ya Zanzibar kutokuwa na mashindano mengi ya michezo mbali mbali, ambayo viwanja vyake vimejengwa kimataifa na vinakidhi viwango vya kuandaa mashindano.
“Ni kweli niseme kwamba tunaweza kujivunia kama tuna viwanja vyenye viwango vizuri na kimataifa ambavyo vinatakiwa kutumiwa kwa utaratibu mzuri”, alisema.
Sambamba na hayo alisema baada ya uzinduzi huo wa awamu ya pili, uwanja huo wa Amaan utakuwa umekamilika kwa kila kitu na kazi iliyobakia ni kufanya matamasha na mashindano mengi ili uweze kutumika.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita alisema Dk. Mwinyi ameacha historia ya mafanikio katika uongozi wa serikali ya awamu ya nane Mapinduzi ya Zanzibar .
Katibu wa wizara hiyo Fatma Hamad Rajab alisema yote hayo yamefanikiwa kutokana na ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka kwa watendaji wao .
Mkarandasi wa uwanja huo Ilhan alisema kazi iliyoifanyika ni kubwa ya kujenga uwanja wa Amaan, viwanja viwili vya nje vya mazoezi, hotel, viwanja vya ndani, maduka, migahawa na uwanja wa Judo.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Idrissa Kitwana Mustafa alisema wananchi wa mkoa wa Mjini wanampongeza sana kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuiletea maendeleo ya nchi yao.
Mwakilishi wa jimbo la Amani Rukia Ramadhan Mapuri alisema wanajivunia sana uwepo wa matengenezo ya uwanja huo ambao umebadilisha mandhari ya mji wao na fahari kubwa ndani ya jimbo lao.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi Talib Ali Talib alisema michezo ni afya kwa binadamu na ajira, hivyo uwepo wa uwanja huo ni matarajio vijana wengi watajiajiri kwa kutumia michezo.
Kabla ya uzinduzi huo rais Mwinyi aliangalia michezo mbali mbali iliyochezwa katika viwanja hivyo ikiwemo mpira wa wavu, kikapu, tennis, ngumi, judo na karate.