Skip to content

Dk. Mwinyi ahudhuria hafla ya maulid Tumbatu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, jana alishiriki kwenye hafla ya maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad yaliyofanyika Tumbatu Jongowe.

Aliwasili kisiwani humo kwa boti ya Kikosi Maalum cha Kuzuaia Magendo (KMKM), ambapo aliungana na waumini na wananchi wa kijiji hicho kwenye hafla ya kisomo cha maulid.

Alipowasili kisiwani Tumbatu, Dk. Mwinyi alipokelewa na viongozi wa dini, serikali, wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama na mamia ya wananchi wa kisiwa hicho kilichopo mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kwenye kisomo hicho vijana kutoka madrasa mbalimbali zilizopo shehia ya Jongowe katika kisiwa hicho walisoma milango ya maulid ikiwa ni kuadhimisha hafla ya kuzaliwa kwa kiongozi wa dini ya kiislam Mtume Muhammad (S.A.W).

Katika hafla hiyo, Dk. Mwinyi aliambatana na viongozi mbalimbali walioongozwa na kaimu mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Idrissa Kitwana Mustafa.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, Mwakilishi wa jimbo la Tumbatu ambaye pia ni mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznaia, Haji Omar Kheir.

Viongozi wengine waliohudhuri ni mawaziri, makatibu wakuu na viongozi wa ngazi mbalimbali.

Mara baada ya kumalizika kwa kisomo hicho waislam wa kisiwa cha Tumbatu walimkabidhi Dk. Mwinyi zawadi maalum ambayo ilikabidhiwa na mwanafunzi wa madrasa, Khamis Mohammed Yahya.