NA MWAJUMA JUMA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameongoza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho kilichofanya uteuzi wa mgombea ubunge wa jimbo la Kwahani na Katibu Mkuu wa Umoja Wanawake Tanzania (UWT).
Kikao hicho kilichofanyika katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui na kumteua Khamis Yussuf Mussa ‘Pele’ kuwa mgombea wa ubunge jimbo la Kwahani katika uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi ya ubunge utakaofanyika Juni 8, mwaka huu na Suzan Peter Kunambi kuwa Katibu Mkuu wa (UWT).
Akitoa taarifa kwa waandishi jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Gabriel Makalla, alisema kikao hicho pia kimezipongeza serikali zote mbili za tanzania na viongozi wake kwa jinsi zinavyoendelea kuwatumikia wananchi.
“Aidha kamati imeipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassan na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa namna zinavyoendelea kuwatumikia wananchi kwa vitendo kupitia utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025”.
Akizungumzia uteuzi wa mgombea wa ubunge, Makalla alisema kuwa uteuzi huo umefanywa baada ya chama kilifikiria na mwisho kuamuwa kumteua Khamis na hilo halitowapa shida kwa sababu wote ni wanachama wa CCM.
Sambamba na hayo akizungumzia kuhusu ACT Wazalendo kujitoa, alisema kuwa hilo wao haliwasumbui na ni imani yao kwamba vipo vyama vyengine ambavyo vitasimamisha wagombea na kushindana nao.
“Sisi tumefanya uteuzi na nafikiri wenzetu wamejitathmini na kuona kwamba labda jimbo hili ni gumu kwao na hawawezi kutupa nguvu zao, lakini vyama vyengine vitakuja kushiriki, tukiamini wanakuja kushindana”, alisema Makalla.
Pele aliteuliwa kushika nafasi hiyo kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Ahmada Yahya Abdulwakil ‘Shaa’ aliyefariki Aprili 8, mwaka huu ambapo mwanzoni mwa mwezi huu Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ilitangaza kufanyika kwa uchaguzi huo mnamo mwezi Juni.
Watati Kamati kuu ikifanya uteuzi wa kuwa Katibu Mkuu wa UWT, Suzan alikuwa Mkuu wa wilaya ya Magharibi ‘A’ akiendelea na jukumu la kukimbiza mwenge wa uhuru uliokuwa wilayani humo baada ya kumaliza kukimbizwa katika wilaya za magharibi ‘B’ na Mjini ambapo leo utakabidhiwa kwa viongozi wa mkoa wa Kaskazini Unguja.