RAIS wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduizi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameziagiza sekta zilizoguswa na Ripoti ya Jiolojia na Utafiti wa Madini kushirikiana na Wizara ya Maji, Nishati na Madini kuyafanyia kazi maeneo yanayowahusu ili ripoti hiyo iwe na tija kwa nchi na watu wake.
Aidha Dk. Amewahimiza wakandarasi wanaofanya kazi za ujenzi wa majengo na kamisheni ya maafa kuitumia ripoti hiyo wakati wa kupangamipango yao ili kunusuru majanga yasitokee.
Alieleza hayo jana katika hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa ndege Zanzibar, wakati akizindua ripoti hiyo na kuzitaka taasisi za mipango miji kuzingatia maeneo yaliyotajwa wakati wanapopanga mji ili kuepusha madhara.
Mbali na hayo alieleza kuwa matumizi sahihi ya ripoti hiyo yatakuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi hivyo wadau wote wanapaswa kuitilia maanani.
Aliongeza kuwa ripoti hiyo itapelekea ajira katika sekta zote husika, huku sekta ya ardhi ikitajwa kuwa itaweka mipangilio mzuri wa matumizi ya ardhi ya kilimo, ujenzi na makaazi na kuiwezesha nchi kuweza kujikinga mapema na maafa kabla ya kutokezea.
Alifafanua kuwa matumizi ya ripoti hiyo yatapelekea ongezeko la uwekezaji katika sekta mbali mbali nchini ambao ni chanzo cha ajira na sekta ya ardhi itaweka mpangilio mzuri wa matumizi ya ardhi ya kilimo, ujenzi, makaazi pia nchi kujikinga mapema na maafa kabla hayajatokezea.
Kwa upande wa Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaibu Hassan Kaduara, alisema utafiti uliozinduliwa ni wa awali lakini yapo maeneo ya bahari ambayo bado hayajafanyiwa utafiti wa kina ikiwemo baharini ambapo hatua iliyobaki ni ya uchambua matokeo ya ripoti hiyo ili kujipanga vyema kwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar na watu wake.
Naye Waziri wa Madini wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Atony Peter Mavunde, alisema hatua hiyo imeiweka Zanzibar katika ramani ya nchi zinazoonekana kuwa uchumi wake unakua kupitia ekta za uchumi wa buluu.
Alisema; “Ukifanyika utafiti wa kina, madini yaliyopo Zanzibar yatasaidia kuinua uchumi wa Zanzibar, ikiwemo ukuaji wa viwanda, upatikanaji wa mali ghafi pamoja na ajira”.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Nishati Zanzibar, Joseph Kilangi, alisema ripoti iliyozinduliwa imehusisha utambuzi wa aina za miamba iliyopo Zanzibar, viashiria vya madini na maeneo vinakojitokeza, maeneo ya mapango ya asili yanayoweza kutumika kama vivutio vya utalii na uwepo wa maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kutokea majanga ya asili.
“Kwa mara ya kwanza serikali imefanya utafiti mkubwa ambao umetoa dira na dalili za kuwepo aina nyengine
za madini hapa Zanzibar na hivyo kuleta mwelekeo mpya wa sekta ya madini kuwa moja ya sekta ambayo ikifanyiwa kazi inaweza kuwa sekta muhimu katika maendeleo ya Zanzibar”, alisema Kilangi.
Alifafanua kuwa utafiti huo ulianza Novemba 20, 2023 na kukamilika Machi 14, 2024, ambapo jumla ya sampuli 189 kutoka maeneo tofauti ya Zanzibar zilichukuliwa na kupelekwa maabara yenye ithibati ya kimataifa ya GST jijini Dodoma kwa uchunguzi wa jiokemia kuainisha madini yaliyopo.
“Miongoni mwa madini yaliyogudulika katika utafiti huo ni pamoja na miamba bora ya chokaa kwa viwanda, madini tembo katika fukwe zote za Unguja na Pemba na miamba inayoweza kuhifadhi maji, mafuta na gesi”, alieleza.
Kilangi aliongeza kuwa utafiti huo umebaini aina nyengine za miamba ya na mawe chokaa, aina kadhaa za mchanga na udongo, uwepo wa viashiria vya madini kama vile ‘strontium’ yanayoweza kutumika kwa utengenezaji wa vioo vya TV.
Alitaja madini mengine kuwa ni ya ‘fireworks’, kromiamu, bariamu, risasi, shaba, valediamu na nikeli ambayo hutumika kwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani, ‘titanium’ yenye sifa ya uimara, wepesi, kuhimili joto na kutofanya kutu yanayotumika kutengenezea maumbo (body) ya ndege, mashine za gari na viungo bandia.