NA MARYAM HASSAN –
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali itaendelea kuhakikisha kwamba bidhaa zinazoingizwa na kuzalishwa nchini zikidhidhi viwango vya ubora.
Dk. Mwinyi alieleza hayo jana mara baada ya kufungua kituo kipya cha ukaguzi wa vyombo vya moto huko, hafla iliyofanyika Maruhubi kwenye ofisi za taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS).
Alisema taasisi zilizopewa dhamana ya kusimamia na kudhibiti ubora wa bidhaa ikiwemo ZBS, zitaendelea kutekeleza wajibu lengo la kuhakikisha Zanzibar haigeuzwi kuwa jaa la bidhaa ambazo hazikidhi viwango ikiwemo vyombo vya moto.
Alieleza kuwa kuna umuhimu wa kuakikisha vyombo vya moto vinavyoingizwa na vilivyopo nchini vinakidhi usalama na ubora, hivyo ni vyema taasisi za udhibiti viendelee kuvikagua na kuthibitishwa ubora kwa ajili ya matumizi ya barabarani.
“Kama tunavyojua vyombo hivi vinapokosa ubora, husababisha kutokea kwa madhara mbali mbali yakiwemo uchafuzi wa hali ya hewa unaotokana na moshi na ajali ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia kupoteza nguvu kazi ya taifa”, alisema.
Alisema serikali inatumia fedha nyingi kwa huduma za matibabu kwa waathirika wa ajali zinazotokea maeneo mbalimbali zinazotokana na ajali za vyombo vya moto.
Dk. Mwinyi alisema kituo hicho cha ukaguzi wa vyombo vya moto cha ZBS, kutatolewa huduma jumuishi ambapo mwananchi ataweza kukata bima ya chombo, kufanya malipo kupitia PBZ na kusajili chombo cha moto kupitia Mamlaka ya Mapato Zanzibar.
Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alisema serikali itaendelea kufanya juhudi na kuchukua hatua kuhakikisha kuwa inajenga miundombinu imara ya kuwezesha kufanya shughuli za usimamiaji wa ubora kuwa za kisasa hapa Zanzibar.
Kwa upande wake, waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, alisema takwimu zinaonesha kuwa uingiaji wa vyombo vya moto umeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Alizitaka mamalaka zinahusika na upasishaji wa vyombo vya moto kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ili malengo ya usalama, ubora na viwango vya vyombo vya moto vinayofika nchini yaweze kufikiwa.
Mbali na hayo aliitaka ZBS kukitunza kituo hicho ili ifikie malengo yaliyosudiwa na serikali, huku akitanabahisha kuwa uwepo wa kituo hicho kitaongeza mapato serikalini.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Yusuph Majid Nassor, alisema lengo la kujengwa kwa kituo hicho ni kuondoa kadhia za wananchi kwenda kwenye taasisi za umma kwa ajili ya kufanya usajili wa vyombo vya moto katika sehemu mbali mbali.
Alisema wameamua kuwaweka pamoja mamlaka zote za upasishaji ikiwemo Benki ya Watu wa Zanzibar, Mamlaka ya Mapato Zanzibar, na Shirika la Bima Zanzibar, lengo ni kukamilisha zoezi la usajili wa vyombo vya moto kwa wakati bila ya kuwa na changamoto yoyote.
Alisema ndani ya kituo cha ukaguzi wa vyombo vya moto imefungwa mitambo miwili yenye uwezo wa kukagua gari 300 kwa siku na itafanya kazi saa 24
Aliwatoa hofu wananchi kuwa gari zote ambazo zitafeli katika ukaguzi watapewa siku 14 kwa ajili ya kurekebisha matatizo ambayo yatagundulika.