NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Tume ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Maboresho ya Kodi, Ikulu Zanzibar iliyofika kujitambulisha.
Katika maongezi na tume hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Balozi Ombeni Sefue na ujumbe wake, Dk. Mwinyi, wamejadili mambo mbali mbali ikiwemo mapendekezo yatakayo zishauri Serikali mbili za SMZ na SMT kuhusu masuala ya kodi.
Aidha Dk. Mwinyi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuteua tume hiyo na kueleza kuwa itasaidia kuimarisha na kubadilisha mifumo ya kodi kwa serikali zote mbili za SMZ na SMT.
Aliongeza kuwa hatua hiyo pia italeta mageuzi kwenye biashara likiwemo eneo la kodi hadi kukamilika kwake.
Kwa upande wake Balozi Sefue, alizishukuru Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuahidi kuipa ushirikiano tume hiyo.
Tume hiyo ilizinduliwa rasmi Oktoba 4, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambapo pamoja na mambo mengine ina lengo la kuangazia changamoto zinazokabili mfumo wa kodi na kutoa mapendekezo yanayoweza kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kuongeza ufanisi wa matumizi yake.
Jambo jengine ni kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa kodi pamoja na kuzingatia njia mpya za kukusanya kodi zitakazosaidia kuongeza mapato ya serikali bila kuweka mzigo mzito kwa wananchi.