RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameitaka kamati ya kitaifa na timu kuu ya kitaalamu ya dira ya taifa ya maendeleo 2050 kukutana na wadau kuchukua maoni yatakaoimarisha rasimu ya dira hiyo ili kupata dira yenye maono ya Watanzania wote kwa miaka 25 ijayo.
Dk. Mwinyi alitoa maelekezo hayo wakati wa uzinduzi wa rasimu ya kwanza ya dira hiyo katika hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege, zanzibar jana.
Alisema ni vyema kwa Tume ya Mipango ikaratibu vyema zoezi la uhakiki wa rasimu hiyo kwa ufanisi na kuisambaza katika vyombo mbali mbali na kuweka mfumo rahisi wa kupokea maoni ya wadau wote.
Aidha alisema dira mpya imelenga maeneo matano yanayokusudia kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye uchumi hilimivu na jumuishi wa kipato cha kati cha juu utakaomilikiwa na makundi yote wakiwemo wanawake.
Alianisha malengo mengine kuwa ni taifa lililoweka kipaumbele cha maendeleo bora ya watu wote wakiwemo watoto, vijana, wanawake na wanaume, kuwa taifa lenye maisha bora na ustawi kwa wote.
“Malengo mengine ni kuwa na taifa lenye mfumo wa utawala jumuishi, ulio wazi na wenye kuwajibika na kuwa taifa taifa linalotunza uoto wa asili, mazingira na rasilimali kwa kizazi kijacho ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi”, alifahamisha Dk. Mwinyi.
Alisisitiza kuzingatiwa kwa misingi thabiti inayopelekea serikali kuandaa dira yenye inayobeba maono na muelekeo wa taifa kwa miaka mingine 25 ijayo ni katiba na kisheria kwa serikali kuandaa mipango ya maendeleo.
Akizungumzia kaulimbiu ya rasimu hiyo isemayo ‘kuelekea taifa lenye ustawi, amani, haki, jumuishi na linalojitegemea’, Dk. Mwinyi, alisema imebeba lengo kuu la taifa ya kuwa ifikapo mwaka 2050 kuwa na taifa lenye ustawi, amani, haki, jumuishi na linalojitegemea katika nyanja zote bila kuathiri ushirikiano uliopo kikanda na kimataifa.
Hivyo aliwasisitiza wananchi na wadau wote katika nafasi zao kushiriki kuhakiki maudhui ya rasimu ya dira hiyo kwani maoni yao ni muhimu katika kuipata dira hiyo.
Aliahidi kuwa utekelezaji wa dira hiyo utakuwa wa tofauti ili waweze kufikia malengo ikiwemo kusimamia na kulinda rasilimali za nchi ikiwemo fedha zinazoenda kwenye miradi na programu za maendeleo na zile zinazoendesha shughuli za kila siku kwenye ofisi zaumma.
Naye Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya kitaifa ya maandalizi ya dira hiyo, Kassim Majaaliwa Majaaliwa, alisema mchakato wa kukusanya maoni ya dira ya taifa ya maenedeleo ilizinduliwa rasmi Aprili 3, 2023.
Alibainisha kuwa kutokana na umuhimu wa kupatiakana dira thabit na viwango, iliundwa timu yenye wajumbe 14 iliyomjumuisha waziri mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa zanzibar na wajumbe kutoka Serikali zote mbili za tanzania (SMT na SMZ).
Alisema kamati hiyo ina majukumu mbali mbali yakiwemo ya kupokea na kuhamasisha makundi mbali mbali kushiriki katika mkakati wa dira 2050 lengo kuu ni kuona mchakato huo unakamilika.
“Katika utekelezaji wa hayo, kamati ilifanya vikao vinne ikiwemo kuwahamasisha wananchi kutoa maoni yao na kwamba kamati itaendelea kushauri timu kuu ya dira kwa lengo la kuhakikisha maudhui ya dira yanakidhi matarajio na maoni ya Watanzania yatakayowagusa kiuchumi na kijamii kwa miaka 25 ijayo”, aliongeza.
Majaliwa na kumpongeza Dk. Mwinyi kwa kushiriki kwenye tukio la uzinduzi wa rasimu hiyo.
Mapema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Professa Kitila Mkumbo, alisema hadi kufikia Oktoba mwaka huu zaidi ya wananchi na wadau 1,00,000 walifikiwa na kutoa maoni yao.
Akizitaja hatua zitakazofuata kuwa ni kupokea maoni katika ngazi ya uhakiki ambapo zoezi hilo litaanza Disemba 14 na litahitimishwa Januari 14, mwakani kwa Waziri Mkuu kupokea rasimu ya pili ya dira iliyoboreshwa kutokana na maoni mapya yatakayojitokeza.
Alitaja hatua zitakazofuata kuwa kati ya Januari na Machi, 2025 rasimu hiyo itajadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika vyombo vya serikali likiwemo Baraza la Mawaziri, kati ya Aprili na Mei itapokelewa, kujadiliwa na kuidhinishwa rasmi na Bunge kabla ya kuzindiliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan mnamo mwezi Juni, 2025.