RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema maadhimisho ya miaka 60 ya elimu bila malipo ni tukio ambalo lenye maana kubwa katika maendeleo na historia ya nchi ya Zanzibar.
Dk. Mwinyi alieleza hayo jana katika kiwanja cha Amani Complex kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya elimu bila malipo, ambapo alisema maendeleo yaliyofikiwa nchini msingi wake ni elimu bila malipo.
Alisema hatua za maendeleo zilizofikiwa hivi sasa ni matokeo ya maono ya viongozi wa serikali kuanzia awamu ya kwanza chini ya muasisi mzee Abeid Amani Karume aliyetangaza elimu bila malipo mara tu baada ya mapinduzi.
Alieleza kuwa ni jambo jema kwa viongozi katika awamu zote walitambua umuhimu wa elimu katika kujenga taifa huru na lenye usawa.
Dk. Mwinyi alisema hatua ya kutangazwa elimu bila malipo imeleta ukombozi wa kweli kwa jamii ya wazanzibari katika kuinua uchumi na kuliletea taifa maendeleo.
Dk. Mwinyi alisema katika kipindi cha miaka 60 Zanzibar, imepiga hatua kubwa za maendeleo katika sekta mbalimbali, kwani kabla elimu bila malipo Zanzibar ilikuwa na skuli 68 ikiwemo moja ya maadalizi, skuli 62 za msingi na skuli tano za sekondari.
Alisema hivi sasa taasisi za elimu zimeenea ambapo zimefikia zaidi ya skuli 1,300 katika ngazi zote na hali ya upatikanaji wa elimu imekuwa ni haki ya msingi kwa kila mzanzibari.
“Ni jambo la kujivunia kwamba elimu bila malipo imeweza kubadilisha maisha ya wazanzibari kwa kuwapatia maarifa, ujuzi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa letu”, alisema Dk. Mwinyi.
Aliieleza hadhara hiyo kwamba dhamira ya serikali ni kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii na kuifikisha Zanzibar ya uchumi wa kati juu, ambapo mkakati mkubwa katika kufikia malengo hayo upo katika kuimarisha elimu.
Alisema vijana wengi wanahitimu katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu za ndani ya nje ya nchi, ambapo kwa miaka 60 ya elimu bila malipo imefungua milango ya fursa za kujiendeleza kielimu na kufikia upeo wa juu wa maarifa na ujuzi.
Alisema serikali imefanya mageuzi mbalimbali kwenye sekta ya elimu, sambamba na kukabiliana na changamoto mbalimbali ambapo lengo lilikuwa ni nchi kuwa na wataalamu wake.
Alisema hivi sasa serikali inakamilisha sera mpya na sheria ya elimu zitakazozingatia mapendekezo hayo muhimu na kwamba utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi utachangia kufikia malengo katika dira ya maendeleo ya 2050.
Alibainisha kuwa maendeleo ya rasilimali watu, ndiyo msingi wa utekelezaji wa dira ya maendeleo, hivyo serikali ina wajibu wa kuhakikisha mifumo ya elimu inaimarishwa ili kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi.
Alisema serikali itaendelea kuhakikisha kwamba sekta ya elimu inapewa kipaumbele cha kwanza, ambapo katika bajeti ya elimu imekuwa ikiongezeka ambapo serikali ya awamu ya nane, imeongezeka bajeti kutoka bilioni 265.5 mwaka 2021/22 hadi kufikia bilioni 851 mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 221.
Alisema takwimu zinathibitisha kuwa ufaulu katika mtihani wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 56.1 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 90.9 mwaka 2023.
Aidha alisema matokeo ya mtihani wa kidato cha sita ya mwaka 2024 yametoa faraja kubwa ambapo asilimia 99.6 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wamepata ufaulu wa kujiunga na vyuo vikuu.