Skip to content

Dk. Mwinyi: Matumizi ya dijitali kuharakisha maendeleo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema hatua zisipochukuliwa katika kuandaa vijana kwenye elimu za kidijitali, kuna uwezekano nchi kubakia kuwa msindikizaji kwenye maendeleo.

Amesema dunia iko kwenye kasi ya matumizi ya kidijitali ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangaia kuharakisha maendeleo kwenye maeneo mbalimbali, hivyo kuna ulazima wa Zanzibar kuwa na wataalam vijana ambao watakwenda sambamba na kasi hiyo.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana huko katika ukumbi wa hoteli ya Madinat Al Bahr, alipokuwa akifungua mkutano wa tatu wa   uliozunguzia matumizi ya teknolojia katika kuongeza ubunifu ili kuchochea uanzishaji wa taasisi changa na zinazoinukia.

“Kutokana na kasi ya maendeleo ya kidigitali ilivyo duniani, bila ya kujifunza na kuitumia teknolojia, nchi yetu inaweza kuwa mshindikizaji na kushindwa kupata maendeleo ya haraka kama zilivyo nchi nyengine”, alisema Dk. Mwinyi.

Aliieleza hadhara hiyo kwamba, mkutano huo unadhihirisha umuhimu wa wataalamu na wajasiriamali kuwa wanahitaji kujifunza zaidi katika maeneo mbali mbali ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.

Dk. Mwinyi alisema kuna umuhimu mkubwa kuwapatia taaluma vijana wanaochipukia katika biashara na uvumbuzi wa teknologia katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, biashara, afya, elimu, tehama ili wasaidie kukua kwa maendeleo.

Alisema vijana wanaochipukia katika ujasiriamali wana umuhimu katika kukuza uchumi jumuishi na endelevu, hivyo kuna haja ya kuwawekea mazingira bora na rafiki ili waweze kuvumbua biashara zenye faida.

Akizungumzia kuhusu utafiti uliofanywa na ZRCP kwa kushirikiana na taasisi za serikali, ubalozi wa Uholanzi, UNDP na USAID, alisema matokeo ya utafiti huo yanatoa ushahidi uwepo wa mazingira wezeshi, vipaji, masoko na upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali hapa Zanzibar.

Aidha alifahamisha kuwa matokeo ya utafiti huo kwa kiasi kikubwa yatasaidia kuainisha teknolojia kwenye sekta ambazo zinastahili kupewa kipaumbele kwenye kukuza ubunifu wa biashara hapa nchini.

Alisema Zanzibar ina wajasiriamali vijana wenye vipaji tofauti ambavyo vinahitaji kuendelezwa na kukuzwa na kwamba ni matumaini yake matokeo ya utafiti huo yatatoa muelekeo wa namna bora ya kujenga mazingira wezeshi.

Alibainisha kuwa nchi nyingi duniani zikiwemo Uholanzi, India, Korea Kusini na baadhi ya nchi za Afrika zinatumia mfumo wa kuendeleza wajasirimali ili kukuza utajiri wa nchi, kuongeza pato la taifa na kutengeneza ajira zenye maslahi.

Kwa kuwa mada zitakazowasilishwa zina umuhimu mkubwa kwa Mustakbali wa taifa letu, ninazielekeza Taasisi zilizoratibu mkutano huu, kuongoza mjadala wa mada zitakazojadiliwa kwa umakini ili zituletee tija hapa nchini.

Alisema ni matarajio yake kwamba wa mapendekezo yatayotokana na mijadala kwenye mkutano huo, yatawasilishwa kwa taasisi na wadau wanaohusika moja kwa moja ili zitengenezewe sera na mipango ya utekelezaji.

Dk. Mwinyi alisema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuziimarisha taasisi za kukuza uchumi ili kuhakikisha vijana wanakuza taaluma zao na kushiriki kikamilifu katika kuvumbua na kuendeleza vipaji nchini.

Alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango na Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji kwa ushirikiano mzuri na taasisi ya tafiti nchini (ZRCP) kwa kuandaa mkutano huo hapa Zanzibar.

Kwa upande wake, waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema utafiti unaofavywa na kituo cha ZRCP una lengo la kuweka msukumo wa kufanikisha malengo ya serikali na kuleta mageuzi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ZRCP, Juma Reli, alisema ZRCP imekusudia kuwa kituo bora chenye kutoa tafiti zenye manufaa kwa jamii katika ukanda wa Afrika Mashariki.