Skip to content

Dk. Mwinyi: Miradi ya maendeleo izingatie wakati

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini inahitaji kuzingatia wakati katika utekelezaji wake ili ilete tija kwa taifa.

Dk. Mwinyi alieleza hayo Ikulu mjini Zanzibar jana alipokutana na ujumbe wa watendaji kutoka Kituo cha Nishati cha Oman uliofika kuelezea hatua za miradi wanayoisimamia hapa Zanzibar ikiwemo miradi ya maji, nishati na ukarabati wa Mji Mkongwe ambao ni urithi wa dunia.

Katika mazungumzo yao, Dk. Mwinyi aliuhakikishia ujumbe huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kufanikisha miradi hiyo aliyoelezea kuwa ina umuhimu mkubwa kwa Uchumi wa Zanzibar, maendeleo na ustawi wa wananchi wake.

Dk. Mwinyi ameueleza Ujumbe huo kutosita kuwasilisha Serikalini vikwanzo na changamoto zozote zitakazojitokeza kwenye utekelezaji wa miradi ili serikali ichukue hatua za haraka kukabiliana nazo.

Akitilia mkazo mradi wa maji safi na salama, Dk. Mwinyi aliushauri ujumbe huo kuweka mazingatio zaidi kwa kuhakikiksha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa maeneo yote yaliyopitiwa na miradi yao.

Aidha alieleza kufarajika kwake kwa muendelezo na utayari wa utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na kituo hicho  hapa nchini ambayo inaendelea kuimarisha ushirikiano na uhusiano baina ya Oman na Zanzibar.

Naye, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo hicho, Abdallah Humaid Al Ma’amary, alisema moja ya maboresho ya Mji Mkonge ni kuufanya kuwa mji wa kisasa (Smart City) bila kuharibu uhalisia wa mji huo na kuzingatia vigezo na miongozo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuwa ni urithi wa dunia na kielelezo muhimu cha historia ya Zanzibar.

Alieleza kuwa tayari wamekamilisha upembuzi yakinifu kwa miradi wanayotarajia kuitekeleza na kusifu ushirikiano wanaoupata kutoka kwa watendaji wakuu wa taasisi za serikali waliopitiwa na miradi hiyo.