Skip to content

Dk. Mwinyi: Serikali inakopesheka

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kwa mujibu wa viwango vya kitaalamu vya kimataifa vya kiuchumi, Zanzibar iko kwenye kiwango kizuri cha kukopesheka.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana ikulu mjini Zanzibar kwenye hafla fupi utiaji saini mkopo euro milioni 79.962, ambazo ni sawa na shilingi bilioni 240, fedha ambazo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekopa kutoka Benki ya CRDB ya hapa nchini.

Alisema kwa mujibu wa viwango vya kitaalam vya pato la nchi na madeni (debt-to-GDP ratio), Zanzibar ina deni la asilimia 17 ambalo ni kiwango kizuri na kinachoonesha nchi inaweza kukopesheka.

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa vigezo hivyo, nchini inahesabiwa kuwa iko kwenye mgogoro pale inapofikia ukopaji wa wastani wa baina ya asilimia 50 hadi 55 kulingana na pato la nchi.

Dk. Mwinyi alibainisha kuwa kwa kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeonesha kuwa Zanzibar inaweza kukupesheka na iko kwenye kiwango cha asilimia 17.

Alisema utekelezaji wa mikakati ya maendeleo inategemea vyanzo vya fedha, ili kufanikisha miradi na kuleta maendeleo kwa wananchi na kwamba umefika wakati wa kuwa na vyanzo vya fedha vitakavyofanikisha utekelezaji wa mikakati.

“Tumebuni njia mbadala kutafuta fedha, kwanza ni Zanzibar SUKUK ambayo tayari tumepata shilingi bilioni 381 na njia ya mikopo kwa benki za ndani, ambapo kwa mara ya kwanza katika historia tunakopa kupitia benki ya ndani”, alisema.

Alisema mikopo aina kama hiyo kutoka CRDB utafungua milango ya utekelezaji wa miradi zaidi ikiwemo ujenzi wa hospitali ya rufaa, hospitali ya saratani, uimarishaji wa bandari ya Mangapwani na miradi ya maji ya maeneo ya Kusini na Kaskazini Unguja na Pemba.

Dk. Mwinyi alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia miradi ya maendeleo kupitia dhamana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba na barabara za Chake-Chake hadi Mkoani, Tunguu hadi Makunduchi na Kisauni hadi Fumba.

Alisema Zanzibar inaingia katika enzi mpya ya kifedha ambapo inaweza kujitegemea zaidi kwa kutumia mbinu za kiuchumi za kitaalamu na kuachana na utegemezi wa vyanzo vya kifedha vya kawaida.

Awali, akizungumza mara baada ya zoezi la utiaji saini Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema ushirikiano kati ya benki hiyo na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni wa muda mrefu na umewezesha mambo mengi kufanyika.

Alieleza kuwa benki hiyo imeguswa na dira ya Dk. Mwinyi hasa wakati wa janga la COVID-19, ambapo aliweka mpango wa kuwainua wajasiriamali kwa mikopo nafuu ya shilingi bilioni 60 zisizokuwa na riba.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Juma Makungu Juma, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Saada Mkuya, alisema hakuna mtu anayepinga kuwa elimu ni msingi wa maendeleo, hivyo mipango yote ya serikali inaanza na uwekezaji kwenye elimu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid.