Skip to content

Dk. Mwinyi: Tunathamini uhusiano wa dhati na China

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Jamhuri ya watu wa China.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na balozi mdogo mpya wa China aliyepo Zanzibar, Li Quanghua, aliyefika ikulu Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha rasmi akiwa ameambatana na ujumbe wake.

Alisema Jamhuri ya Watu wa China imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika nyanja mbalimbali, ikiwemo sekta ya afya ambapo kila mwaka nchi hiyo inaleta timu ya madaktari wanaokuja nchini kutoa huduma za kibingwa katika hospitali za umma

Aidha Dk. Mwinyi alisema nchi hiyo pia imekuwa ikiwapatia Wazanzibari fursa za ufadhili wa masomo hatua ambao inasaidia Zanzibar na wataalamu ake wa ndani kwenye fani mbalimbali.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Mwinyi ametaja maeneo mahususi ya ushirikiano ambayo serikali ya Zanzibar imeyapa kipaumbele, yakiwemo: kuhamasisha uwekezaji kutoka China, kukuza biashara baina ya pande mbili.

Eneo jengine ni kuimarisha programu za kuwawezesha vijana kupitia mafunzo ya ufundi stadi ili kupunguza changamoto ya ajira hasa kwa vijana wanaokosa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika sekta ya utalii, hususan kwa kuangazia uwezekano wa kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja za ndege kati ya China na Zanzibar.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza idadi ya watalii, kukuza mahusiano ya kitamaduni na kuimarisha uchumi.

Kwa upande wake, Balozi Li alimshukuru Dk. Mwinyi kwa ukarimu mkubwa alioupokea tangu alipowasili na kueleza kuwa katika kipindi kifupi alichokuwepo Zanzibar, ameweza kutembelea miradi mbalimbali na kuridhishwa na kasi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.