RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi,amesema ukaguzi una mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Dk. Mwinyi alieleza hayo katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya ukaguzi yaliyofanyika katika ukumbi wa Polisi Ziwani na kueleza kuwa hadi mwaka 2023 kasi ya ukuaji wa uchumi imefikia wastani wa asilimia 7.4 ikilinganishwa na asilimia 1.3 ya mwaka 2020.
Alisema mafanikio ya kazi za ukaguzi wa rasilimali za umma, yameimarsha utoaji huduma za kijamii zikiwemo za elimu, afya, maji safi na salama, nishati ya umeme na huduma nyengine.
Aliongeza kuwa ukaguzi wa rasilimali fedha na rasilimali nyegine umefanikisha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, viwanja vya michezo na masoko katika kipindi kifupi.
Aidha alipongeza jitihada zinazochukuliwa na ofisi ya CAG katika kuimarisha utawala bora wenye kuzingatia uwajibikaji, uwazi na nidhamu katika matumizi ya rasilimali za umma ambazo zina mchango mkubwa katika kusukuma ajenda za maendeleo.
Alisema serikali itaendelea kuijengea mazingira mazuri ofisi hiyo itekeleze kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo kitaifa na kimataifa ili kwenda sambamba na mabadiliko ya mara kwa mara ya ukaguzi duniani.
Dk. Mwinyi alipongeza ushirikiano uliopo baina ya ofisi ya CAG na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ya Tanzania katika kufanikisha kazi za ukaguzi wa hesabu za serikali nchini kwani ushirikiano ni ishara ya uimara wa muungano wa Tanzania bara na Zanzibar ulioasisiwa mwaka 1964.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alisema ofisi hiyo ina mabadiliko makubwa yanayotokana na kusimamiwa vizuri na bodi ya ushauri ya taasisi hiyo na kuwataka wale waliopatiwa majukumu kuyasimamia vizuri ili lengo la kuwepo kwa ofisi hiyo lifikiwe.
Waziri Haroun, alimpongeza Dk. Mwinyi kwa jitihada anazozichukua katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar na anaamini Zanzibar itapiga hatua kubwa za maendeleokatika miaka michaache ijayo.
Awali Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, Dk. Othman Abass Ali, alisema utaratibu wa kusomwa kwa taarifa ya ukaguzi wa hisabu za serikali hadharani na kujadiliwa kwa kina katika Baraza la Wawakilishi umeleta mafanikio makubwa na kujenga uelewa wa wananchi juu ya matumizi ya fedha za umma.
Alitaja mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushauri unaotolewa na ofisi yake, ni pamoja na kuanzishwa kwa mifumo ya kifedha serikalini iliyomeleta tija kwa kuokoa fedha za serikali kwa wastani wa asilimia 90.
Alibainisha kuwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa uwazi kwa wastani wa asilimia 96.8, kuongezeka kwa uelewa wa usimamizi wa fedha za umma kwa wastani wa asilimia 98 na matumizi ya mifumo kwenye shughuli za serikali imeongezeka kutoka asilimia 48 hadi kufikia wastani wa asilimia 97.4
Alisema maadhimisho ya siku ya ukaguzi ni fursa kwa taasisi za umma kuwatumia wataalamu wao kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu za kukabiliana na vitendo vya rushwa, uhujumu uchumi na kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Alisema katika kulifikia lengo hilo jitihada za makusudi lazima zichukuliwe na serikali kuzijengea uwezo taasisi za utawala bora kwani taasisi hizo zinatoa mchango mkubwa wa kuyafikia matarajio ya serikali na kumpongeza Dk. Mwinyi kwa jitihada anazozichukua katika kusimama misigi na utawala bora na kuimarisha kwa uwajibikaji katika taasisi za umma.
Maadhimisho ya wiki ya ukaguzi ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Zanzibar kwa mwaka 2024, yenye kauli mbiu isemayo, ‘Kuimarika kwa Ukaguzi wa Rasilimali za Umma Kunaongeza Ufanisi na Kuleta Tija Nchini’ yalianza Disemba 12 kufikia kilele chake jana yaliambatana na shguhuli mbali mbali hapo kabla.