Skip to content

Dk. Mwinyi: Zanzibar kunufaika zaidi na uzoefu wa Indonesia

NA MWANDISHI WETU, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduizi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar itanufaika kwa kiasi kikubwa kupitia uzoefu iliyo nao Indonesia hasa kwenye sekta ya mafuta na gesi, uchumi wa buluu, kilimo cha zao la karafuu na mwani.

Dk. Mwinyi alieleza hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) baada ya kuwasili nchini akitokea ziarani nchini Indonesia na Msumbiji.

Alifahamisha kuwa serikali imewakaribisha nchini wawekezaji kutoka Indonesia kuja kuangalia maeneo ya uwekezaji hasa kwenye sekta hizo tatu muhimu ambazo bado zina fursa pana zaidi za kuwekeza.

Akizungumzia suala la mafuta na gesi, Dk. Mwinyi alisema uzoefu iliyonayo Indonesia kwenye sekta ya uchimbaji wa mafuta na gesi kumeivutia Zanzibar kupata uzoefu huo na tayari imeikaribisha kampuni ya Peltamina inayomilikiwa na serikali ya nchi hiyo kuangalia uwezekano wa uchimbaji wa Mafuta na gesi.

Alifahamisha kuwa sekta hiyo imepiga hatua kubwa nchini Indonesia kwa kufanya kazi hiyo na nchi mbali mbali duniani ambapo kuhusu zao la alisema serikali imeingia makubaliano na Indonesia kuja kuangalia uwezekano wa kuchakata bidhaa za karafuu kwa kuziongezea thamani.

“Mpango wetu ni kuanzisha vikundi vya wajasriamali vya akina mama kwa dhamira ya kuwa na vituo vya kuchakata majani ya karafuu lakini kuhusu utalii, serikali ya Indonesia imekubali kutoa fursa za mafunzo kwa vijana wa Zanzibar kwenda Indonesia kujifunza masuala ya utalii”, alieleza Dk. Mwinyi.

Dk. Mwinyi ambaye alihudhuria mkutano wa jukwaa la pili la ushirikiano kati ya Indonesia na Afrika ambapo alimuwakilisha rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, dk. Samia Suluhu hassan na kushiriki katika mikutano na shughuli mbali mbali zilizolenga kukuza uwekezaji na uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.