Skip to content

Dk. Samia ahimiza amani, usalama DRC na Rwanda

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amezisisitiza nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za kumaliza uhasama uliopo baina ya DRC na Rwanda chini ya mchakato wa Angola.

Wito huo ulitolewa kwa niaba yake jana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyialipokuwa akifungua mkutano wa dharura wa Wakuu  na Serikali wa  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika katika ukumbi wa bunge la Zimbabwe, jijini Harare Zimbabwe.

Dk. Samia ambaye ni Mwenyekiti wa asasi ya siasa, ulinzi na ushirikiano wa usalama ya SADC, alifahamisha kuwa upo umuhimu wa kuandaa mikakati madhubuti itakayoainisha juhudi zinazoendelea za kijeshi chini ya SAMIDRC  na za kidiplomasia chini ya Angola zenye lengo la kumaliza mzozo huo.

Alieleza kuwa inapaswa kuwepo mikakati itakayohakikisha amani na usalama  inakuwa endelevu mashariki mwa DRC na nchi wanachama zinapaswa kushirikiana na kutoa kipaumbele kwenye masuala ya amani, maendeleo na ustawi katika ukanda wa SADC.

Aidha aliwaeleza viongozi waliohudhuria mkutano huo kuelewa kwamba hali ya ulinzi na usalama mashariki mwa DRC haijatengamaa kutokana na kuripotiwa kwa mashambulizi yanayofanywa na makundi yenye silaha.

Alisema makundi hayo yamekuwa yakisababisha vifo, kuzorota kwa utoaji wa misaada ya kibinadamu, raia kupoteza makaazi na ongezeko la idadi ya wakimbizi.

Alisema maazimio yatakayofikiwa katika mkutano huo yatakua chachu ya kuchagiza juhudi za kuleta amani ya kudumu katika ukanda wa SADC hususani nchini DRC.

Aidha Dk. Mwinyi alisema utekelezaji wa maazimio hayo ni ushahidi wa dhamira ya kuhakikisha jumuiya hiyo inaondokana na changamoto mbalimbali zinazotishia hali ya amani na usalama.

Alieleza kwamba licha ya changamoto ya kifedha, nchi wanachama zina wajibu wa kusaidiana katika kukabiliana na changamoto za ukosefu amani na usalama kama ilivyoanishwa katika itifaki na nyaraka muhimu za kisheria za SADC.

Alisema kwa lengo la kuhakikisha juhudi zinazotekelezwa na kanda zinaleta mafanikio yaliyokusudiwa, kuna umuhimu wa kuandaliwa mipango itakayoanisha juhudi zinazoendelea za kijeshi chini ya SAMIDRC na za kidiplomasia chini ya mchakato wa usuluhishi unaongozwa na nchi ya Angola.

Alisisitiza kwamba wakati nchi za SADC zikiendelea kujadiliana kuhusu hali ya usalama nchini DRC, ni vyema ikaekwa mifumo ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maazimio yanayoidhinishwa na Jumuiya za kikanda kwa lengo la kuzisaidia misheni ikiwemo ya Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN).

Alisema hatua hiyo itawezesha kupatikana kwa misaada ya kifedha na kilojistiki kwa wakati, kuongeza ufanisi kwenye misheni na kupunguza gharama za uendeshaji.

“Natambua kuwa sekretarieti ya SADC inaendelea kuwasiliana na washirika wa maendeleo (ICPs) katika kufanikisha upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya SAMIDRC. Tuendeleze juhudi hizo ili tuweze kuisadia misheni yetu”, alisema.

Pamoja na hayo, Dk. Mwinyi alisisitiza azma ya Tanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za kumaliza uhasama uliopo baina ya DRC na Rwanda zinazoratibiwa na chini ya msuluhishi Rais wa Angola, Joao Manuel Lourenço.

Alisema kwa madhumuni ya kupata uelewa kuhusu mchakato wa amani wa Angola, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amemualika rais Lourenço ili kutoa taarifa ya kina kuhusu hatua iliyofikiwa baina ya DRC na Rwanda.

Aidha aliwaarifu viongozi hao kwamba Tanzania tangu ichukue uenyekiti wa SADC Organ, imekuwa na jukumu la kuongoza misheni za uangalizi wa chaguzi za SADC (SEOMs) zilizofanyika Msumbiji, Botswana, Mauritius na Namibia.

Ufunguzi wa mkutano huo, ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Rais Lazarus Chakwera wa Malawi, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Antoine Tshisekedi, Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Paul Mashatile na viongozi wengine wa ngazi mbali mbali wa nchi za SADC.