TANZANIA na Umoja wa Ulaya (EU) zimekukubaliana kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kwa kwa kuongeza upatikanaji wa masoko katika umoja huo kwa bidhaa za Tanzania na kuvutia uwekezaji kwenye sekta za kimkakati kama nishati jadilifu na viwanda.
Hayo yalisemwa jana jijini hapa katika hafla ya utiaji saini wa tamko la pamoja kama alama ya makubaliano ya kuendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo kwa maslahi ya pande zote mbili.
Akizungumza kwa naiba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Naibu Waziri wizara hiyo, Cosato Chumi, alisema wamejadili kwa kina masuala muhimu yanayogusa maslahi ya pande zote mbili ikiwa ni pamoja utawala bora, demokrasia, usalama wa baharini,biashara na uwekezaji,ulinzi na usalama kikanda na kimataifa.
Alisema maazimio yaliyofikiwa katika majadiliano hayo ni kuimarisha ushirikiano wa kibiashara ambapo Tanzania na Umoja wa Ulaya zimeeleza dhamira yao ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa pande mbili chini ya mkataba wa Samoa.
Kuhusu biashara na uwekezaji alisema katika kutambuaumuhimu wa sekta hizo, pande zote mbili zimekubaliana umuhimu wa kuongeza upatikanaji masoko ya Umoja wa Ulaya kwa bidhaa za Tanzania na kuvutia uwekezaji zaidi.
“Kwa sasa Umoja wa Ulaya umewekeza miradi ya utalii na miundombinu yenye thamani ya Euro bilioni tatu sawa na shilingi tirioni 8.3, kwa usalama wa baharini kwa pamoja tumezungumza na kujadiliana kuimarisha ushirikiano wa kukabiliana na changamoto za usalama kama uvuvi haramu,usafirishaji haramu wa bidhaa na uharamia,”alisema.
Kuhusu amani na usalama kikanda, alisema majadiliano hayo waliangazia majadiliano ya nchi kama Mwenyekiti wa asasi ya siasa ulinzi na usalama wa SADC, mchango wake katika Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pia wamekubaliana kuendelea kuimarisha juhudi ya kukabiliana na changamoto za kulinzi na kiusalama katika ngazi za kikanda na kimataifa.
Alisema ushirikiano huo unaendana na dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2020/2025 na mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano.
Alisema pande zote mbili zimekubaliana kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha matokeo chanya na yenye manufaa kwa wananchi.
Aliushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada wake endelevu kupitia mfuko wa mpango wa maendeleo na ushirikiano wa kimataifa ambao umeweka euro milioni 726 ambazo zimewezesha utekelezaji miradi miwili katika sekta za nishati, uchumi wa buluu, mabadiliko ya tabianchi na mpango wa miji kuwa kijani.
Alieleza katika majadiliano hayo Tanzania imesisitiza kuendeleza misingi ya utawala bora na demokrasia akitumia fursa hiyo pia kueleza mabadiliko muhimu yaliyofanyika falsafa ya 4Rs.
Alisema majadiliano hayo yameonesha hatua nyinginemuhimu ya kuimarisha ushirikiano madhubuti ambao Tanzania na Umoja wa Ulaya zimeudumisha tangu mwaka 1960.
“Tanzania ikiwa ni moja ya nchi wanachama wa kundi la Afrika, Caribbean na Pacific inaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kushiriki kikamilifu katika majadiliano muhimu kila mwaka kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Umoja wa Ulaya,” alisema Naibu Waziri.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia kanda ya Afrika, Balozi Ritha Laranjinha alisema umoja huo umekubali kuimarisha ushirikiano na Tanzania kwa kuheshimu miongozo ya mkataba wa Viena juu ya uhusiano ya kidiplomasia .
Alisema wataendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika usalama wa bahari huku EU ukiahidi kuendelea kuchangia juhudi za upatikanaji wa amani katika ukanda wa Afrika na dunia kwa ujumla.