Skip to content

G7 yaeka kikomo matumizi ya makaa ya mawe

TURIN, ITALIA

MAWAZIRI wa nishati kutoka nchi saba zilizostawi zaidi kiviwanda (G7), walimaliza makutano wao wa siku mbili, ambapo katika miongoni mwa mambo waliyoazimia ni kuachana matumizi ya makaa ya mawe.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo inasema kuwa nchi za G7 zitasitisha matumizi ya makaa ya mawe katika uzalishaji wa umeme ifikapo katikati ya miaka ya 2030.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya nchi hizo katika kuzuia ongezeko la joto duniani ambalo limekuwa likisababisha athari mbalimbali.

Taarifa hiyo pia inatoa wito kwa nchi nyengine kuwasilisha malengo yao mapya ya kupunguza uzalishaji wa hewa zinazochafua hali ya hewa kwa mwaka 2030 na kuendelea, ifikapo mapema mwaka ujao.

Aidha G7 zilieleza kuwa zinalenga kuongeza mara tatu uwezo wa kimataifa wa kuzalisha nishati mbadala ifikapo mwaka 2030.

Nchi hizo zinaweka lengo la kuongeza hifadhi ya nishati zaidi ya mara sita hadi gigawati 1,500 kutoka viwango vya sasa kupitia betri na njia zingine.

Taarifa hiyo pia inasema nchi za G7 zitaongeza ushirikiano katika kuunga mkono nchi zinazoendelea barani Afrika na maeneo mengine kwa ajili ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.