NA KIJA ELKIAS, MOSHI
MKUTANO wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliokuwa ukiongozwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho Taifa, CPA Amos Makalla, ulivurugika kwa muda baada ya helikopta kutua katika uwanja wa Soko la Manyema, Manispaa ya Moshi uliokuwa ukifanyika mkutano huo.
Tukio hilo lilisababisha wananchi waliokuwa wakifuatilia hotuba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, kuacha mkutano na kukimbilia eneo ilipotua helikopta hiyo kwa ajili ya kupiga picha na kushangiria, jambo lililosababisha mkutano kusimama kwa muda.
Helikopta hiyo iliwasili kwa agizo la Diwani wa Kata ya Bomambuzi, Juma Raibu, ambaye alisema alikusudia kuleta hamasa kwa wananchi kuhudhuria mkutano huo, hata hivyo, uamuzi huo haukupokelewa vyema na viongozi wa chama na serikali, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu.
“Nilikuwa nimepanga helikopta ije saa 8:00 mchana, sambamba na kuwasili kwa mgeni rasmi, lakini kulikuwa na ucheleweshaji wa mawasiliano, sikudhamiria kabisa kuvuruga mkutano,” alisema.
Kwa mujibu wa mashuhuda, helikopta hiyo ilipowasili iliingiza kelele na kutifua vumbi kubwa lililosababisha Boisafi kusitisha hotuba yake kwa muda, huku jeshi la polisi likimuagiza rubani wa helikopta hiyo kuondoka mara moja.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Nurdin Babu, alionekana kutofurahishwa na tukio hilo na kumuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) kufuatilia suala hilo na kubaini waliohusika.
“Hatupaswi kuruhusu vitendo vya kuvuruga mikutano ya kitaifa, hasa yenye lengo la kuwaeleza wananchi sera za chama na serikali,” alisema Babu kwa ukali.
Baada ya helikopta kuondoka, mkutano uliendelea kama kawaida na wananchi walirejea kuendelea kumsikiliza Makalla na viongozi wengine wa CCM waliokuwa wakihutubia.