Skip to content

JKT yawaita vijana bara , visiwani kujisajili

NA SAIDA ISSA, DODOMA 

JESHI la Kujenga Taifa (JKT), limewaita vijana wote wa Tanzania Bara na Visiwani, kujiunga na nafasi za mafunzo ya jeshi hilo, kwa kujitolea huku wakiwatahadharisha wananchi kuepuka matapeli kwani nafasi hizo hazilipiwi ni bure. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabale, Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala (JKT) Kanali Juma Mrai alisema utaratibu wa Vijana kujiunga na hatimaye kuchaguliwa na mafunzo hayo unaratibiwa na ofisi za wakuu wa Mikoa na Wilaya ambapo mwombaji anaishi. 

“Usaili wa Vijana kujiunga na mafunzo ya jeshi la kujeunga Taifa kwa kujitolea utaanza Oktoba 01, 2024 kwa Mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani,

“Vijana watakaoteuliwa watatakiwa kuripoti kwenye makambi ya jeshi la kujenga Taifa kuanzia Oktoba1 Novemba 2024 hadi Novemba 3 ,2024,”alisema Kanali Juma Mrai. 

Aidha alisema Jeshi la kujenga Taifa linapenda kuwataarifu Vijana watakaopata fursa hiyo kuwa jeshi la kujenga Taifa kuwa halitoi ajira, pia halihusiki kuwatafutia ajira katika Asasi, vyombo vya ulinzi na Usalama na mashirika mbalimbali ya Serikali na ya sio ya kiserikali. 

“Hivyo ifahamike kwamba Jeshi hutoa mafunzo ambayo yatawasaidia Vijana kujiajiri wenyewe Mara baada ya kumaliza mkataba wao na jeshi la kujenga Taifa JKT, “alisema Kanali Mrai. 

Sifa za mwombaji na maelekezo ya vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo yatapatikana katika Tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz.