WAFANYABIASHARA wa soka la Jumbi wana wajibu wa kufuata taratibu, miongozo na sheria za serikali wakati wa kuhamia soko jipya.
Kauli hiyo ilitolewa na katibu wa Jumuiya ya wafanyabiashara na wajasiriamali wa soko la Jumbi (JUWASOJU) Faki Suleiman Khatib, wakati wa mkutano wa wafanyabiashara hao uliofanyika soko la Jumbi.
Alisema wakati wafanya biashara hao wanatarajiwa kuhamia soko jipya hivi karibuni, serikali itatoa miongozo na utaratibu kwa wale wote watakao hamia, hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanaifuata ili kuondosha ufumbufu.
Alisema serikaki imetumia pesa nyingi kujenga soko hilo, hivyo si vyema baada ya muda mchache kila kitu kinaharibiki kwa kushindwa kufuata utaratibu ambao serikali itauweka.
“Wafanyabiashara wote wanatakiwa kuanza maandalizi ya kujiandaa kuhamia soko jipya, lakini huko kutakuwa na miongozo ambayo itatolewa tuwe tayari kuifuata’’, alisema.
Aidha aliwatoa hofu kuwa katika kuhamia soko hilo kuwa hakuna hata mfanya biashara mmoja atakayeachwa, hivyo waachane na maneno ambayo yameanza kujitokeza hivi sasa, ambayo hayana nia njema na yana lengo la kutaka kuleta mfarakano.
“Kumekuwa na maneno mengi hivi sasa kuhusu soka jipya, wapo wanaosema kuwa wataletwa wafanya biashara wengine sisi tutaachwa jambo hili sio kweli, na ukweli ni kuwa hakuna hata mfanyabiashara mmoja atakayeachwa hilo nawahakikishia’’, alisema
Kuhusu kulipa kodi aliwataka wafanyabiashara hao kuacha tabia ya kukwepa kulipa kodi, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaikosesha serikali mapato.
Alifafanua kuwa kumekuwa na baadhi ya wafanyabiashara ambao hufanya udanganyifu wa kuweka vikwazo katika kulipa kodi, jambo hilo halitapewa nafasi wakati wa kuhamia soka jipya.
Wakitoa michango yao katika mkutano huo waliiomba serikali kuweka utaratibu mzuri kwa wafanyabishara bila ya upendeleo wakati wa kuhamia soka hilo ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.