KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, imesema imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa majengo ya utawala, taaluma na makaazi ya wanafunzi (mabweni) yanayojengwa katika Taasisi ya Sayansi za Bahari iliyopo Buyu Zanzibar.
Akiongoza ujumbe wa Kamati hiyo iliyokwenda sambamba na ukaguzi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) huko Buyu, Mwenyekiti wa kamati hiyo Husna Sekiboko, alisema matumizi ya kiasi cha shilingi bilioni 11 zilizoidhinishwa katika bajeti zinaendana na thamani halisi ya ujenzi unaoendelea.
Alisema utekelezaji wa mradi huo ulioanza mwezi Febuari 2024, unatarajiwa kukamilika katika miezi 18 ni kutimiza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuimarisha miundombinu ya sekta ya elimu Tanzania.
Hivyo, alisema ni vyema kuendeleza malengo hayo ili kuona lengo linafikiwa sambamba na kuwanufaisha wahusika ambapo lengo la viongozi hao liweze kufikiwa.
“Kwa kweli viongozi wa Chuo kikuu cha Dar es salama mnaendelea kuchapa kazi kwani sisi kamati tumeridhishwa na utekelezaji wa mradi huu ambapo munaendelea kufikia lengo lilliokusudiwa”, alisema Sekiboko.
Naye, Naibu Waziri Elimu Sayansi na Teknolojia, Omar Kipanga, alisema mradi huo unaosimamiwa na Chuo Kikuu Cha Dar esalam, ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa vyema nchini.
Hata hivyo, aliupongeza uongozi wa chuo hicho kwa jitihada zao mbalimbali wanazozifanya kuona elimu inaendelea kuimarika siku hadi siku kupitia chuo chao.
Mapema, Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho Mipango, Fedha, na Utawala, Profesa Bernadeta Killian, alisema ujenzi huo umezingatia mahitaji muhimu ambayo yataimarisha utoaji wa taaluma bora kwa watakaojiunga na masomo.
Alisema ujenzi huo pia unahusisha jengo la utawala na taaluma, ofisi ya Mkuu wa chuo ofisi za walimu, maabara na madarasa huku ikizingatiwa mahitaji ya watu wa makundi yote ikiwemo wenye mahitaji maalum.