Skip to content

Kamati yawasilisha ripoti ukatabati Beit Al Ajaib

NA ASIA MWALIM

KAMATI zinazosimamia majengo ya kihistoria katika Mji Mkongwe wa Zanzibar, zimesema taratibu za kurejesha jengo la Beit Al Ajaib, zinaendelea hatua kwa hatua ili kupata jengo linalokidhi viwango na ubora unaohitajika.

Waliyasema hayo katika kikao kilichokutanisha kamati hizo na uongozi wa Mji Mkongwe, huko ofisi za Mamlaka ya Mkongwe Forodhani mjini Zanzibar.

Mwenyekiti wa kamati ya sayansi ya Mji Mkongwe, Yasser De Costa, alisema ujenzi huo uko tofauti na majengo mengine yaliyozoeleka, kwani unahitaji taratibu maalumu na mbinu za kisayansi.

Aidha alisema jengo hilo litachukua muda kidogo hadi kukamilika kutokana na ulazima wa kurejesha jengo sawa kama lilopromoka awali.

“Jengo hili la kihistoria ni la aina yake, kuanzia msingi, nguzo, kuta na milango yake litarudi katika hali yake ya awali baada ya kufanyika kazi kubwa”, alisema De Costa.

Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali kwa msisitizo wake ya kutunza majengo yote ya Mji Mkongwe kwa faida ya nchi na vizazi vijavyo na kuishukuru serikali ya Oman kusaidia serikali kukarabati jengo hilo.

Mwenyekiti huyo alisema jengo la Beit Al Ajaib lilijengwa mwaka1883 na kupewa jina hilo, kwani ni jengo la kwanza Afrika na baadhi ya nchi dunia lililokuwa na huduma za maji, umeme na lifti.

Nae mwenyekiti wa kamati endeshi Mji Mkongwe, Mwanaidi Saleh Abdallah, alisema lengo la ukaguzi huo ni kupanga mikakati ya ujenzi kwani utengenezaji wake ni mgumu unaohitaji uvumilivu.

Alisema jengo hilo utengenezaji wake ni mgumu na unahitaji uchunguzi wa hali ya juu, hivyo wananachi hawapaswi kulalamika kuchelewa kukamilika ujenzi huo.

Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe, Ali Said Bakari, alisema uwepo wa kamati hizo ni maelekezo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa lengo la kuishauri Mamlaka ili maeneo hayo kuendelea kuwa urithi wa dunia.

Alisema wataendelea kushirikiana na kila baada ya muda watatoa taarifa za ujenzi wa jengo hilo, ambalo liliporomoka na sasa linafanyiwa matengenezo ili kurejesha jengo hilo ambalo ni miongoni mwa vivutio vya utalii.

Sambamba na hayo aliwataka wananchi kuendelea kuwa na subira ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuchukua miaka mitatu hadi kukamilika.