Skip to content

NAIROBI, KENYA

MVUTANO baina ya makanisa na serikali umeendelea kutokota nchini Kenya, ambapo kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini humo kanisa katoliki limekataa mchango wa takriban dola 40,000 uliotolewa na rais William Ruto.

Ruto aliitoa pesa hizo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya kasisi na zawadi kwa kwaya wakati alipohudhuria misa ya Jumapili katika kanisa katoliki la Soweto liliopo jijini Nairobi.

Msaada huo ulifuatia kauli ya hivi majuzi ya maaskofu wa kanisa katoliki, walioisuta serikali kwa kushindwa kutekeleza ahadi ilizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Makanisa yamekuwa chini ya shinikizo mwaka huu kutoka kwa vijana wanaopinga nyongeza ya ushuru ambao wamewashutumu kwa kuwa karibu sana na wanasiasa.

Kufuatia mchango wa Ruto uliotangazwa sana Jumapili, wakenya wengi walihimiza kanisa katoliki kukataa pesa hizo.

Rais alikuwa ametoa takriban shilingi milioni 2.6 tasilim za Kenya ambapo aliahidi fedha zilizobaki zitatolewa baadaye, huku pia akiahidi kuipa parokia hiyo basi.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki la Nairobi, Philip Anyolo, alisema pesa hizo zitarejeshwa kwa sababu ya masuala ya kimaadili na hitaji la kulinda kanisa dhidi ya kutumiwa kwa madhumuni ya kisiasa.

Pia alikataa ahadi zake nyingine na kusema mchango wa shilingi 200,000 za Kenya uliotolewa na gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja ambaye alihudhuria ibada hiyo hiyo, pia zitarudishwa.

“Kanisa katoliki linakataza vikali matumizi ya hafla za kanisa kama vile kuchangisha pesa na mikusanyiko kama majukwaa ya kujitangaza kisiasa,” Askofu Mkuu Anyolo alisema.

Uhusiano wa muda mrefu kati ya makanisa na taasisi za kisiasa – katika nchi ambayo zaidi ya 80% ya wakazi ni Wakristo – inaonekana kuyumba, ambapo miaka mitatu iliyopita, makanisa yaliyoanzishwa yalipiga marufuku wanasiasa kutumia mimbari wakati wa ibada kwa malipo ya michango.

Kanisa larejesha mchango wa fedha za Ruto