NA HAWA ALLY
TIMU ya KMKM SC imesema kutokuwepo kwa wachezaji wake wanne wa kikosi cha kwanza ni miongoni mwa sababu zilizopelekea kupoteza mchezo wao wa kwanza wa ligi kuu.
KMKM SC ilijikuta ikipachikwa bao 1-0 dhidi ya maafande wenzao wa Mafunzo SC katika muendelezo wa ligi hiyo mchezo uliochezwa juzi katika uwanja wa Amaan nje.
Akizungumza na gazeti hili kocha msaidizi wa timu ya KMKM SC Ibrahim Khamis alisema wachezaji hao wanne kutokuwepo kumepelekea kupanga wachezaji wengine ambao hawakuwa katika hesabu za kuwa katika kikosi cha kwanza.
Alisema licha ya hivyo lakini timu yake haina muunganiko mzuri kati ya wale wapya na wazamani kutokana na kuchelewa kufanya mazoezi ya pamoja.
“Timu haikucheza vibaya sana, lakini tulikosa mazoezi ya pamoja kati ya wale wapya na wachezaji wa zamani, na hii kwakuwa walichelewa kuripoti katika mazoez”alisema.
Hata hivyo watahakikisha wanayafanyia kazi mapungufu yote ambayo ameyaona katika mchezo huo.
Kocha msaidizi wa Mafunzo SC Abdallah Bakari alisema kupata ushindi katika mchezo wa kwanza wa ligi unatia matumaini kwa wachezaji na benchi lao la ufundi.
Alisema wamecheza mchezo mgumu dhidi ya KMKM SC ambapo kila timu inajua uwezo wa wapinzani wao.
Alisema ushindi huo haukutokana na bahati mbaya lakini ni jitihada kubwa za wachezaji kuhakikisha hawafanyi makosa hasa katika mchezo huu wa kwanza.
Hata hivyo alisema kupitia mchezo huo yapo mapungufu kadhaa ambayo ameyaona katika safu yake ya ulinzi hivyo atayafanyia kazi.