Skip to content

Kwa nini India inapambana na mzozo wa ubakaji?

PAMOJA na changamoto mbali mbali zinazowakabili wakaazi wa mji mkuu wa Kolkata, ambao ndio mkubwa katika jimbo la West Bengal, hawajasitisha maandamano ya kudai haki dhidi ya vitendo vya ubakaji vilivyokithiri katika taifa hilo.

Changamoto hizo zikiwemo za hali ya hewa ya mvua, halijazuia chama cha West Bengal Junior Doctors Front na raia wa matabaka mbalimbali kushiriki katika maandamano makubwa ya kudai haki kwa daktari ambaye alibakwa na kuuawa katika chuo cha matibabu cha RG Kar mwezi uliopita.

Ni zaidi ya siku 36 zimepita tangu daktari huyo kuuawa katika chuo kimoja kikongwe zaidi cha matibabu nchini humo, ambapo tangu kutokea kwa tukio hilo, maandamano yameshika kasi Kolkata.

Waandamanaji hao wanadai haki na kufanikiwa kusababisha kutimuliwa kwa kamishna wa polisi wa jiji hilo na maofisa wa afya wa serikali ya jimbo. Hasira ya umma imeenea kote nchini na pia kwa miji 25.

Katika hotuba ya siku ya uhuru mwezi uliopita, waziri Mkuu Narendra Modi aligusia uhalifu huo, akisema serikali za majimbo zinapaswa kuingiza hofu ya adhabu kwa wahalifu na kuongeza imani kwa jamii, lakini chama chake cha BJP kinaonekana kukabiliana na shida yake ya ubakaji.

Bado, kile kilichotokea usiku wa Agosti 9 mwaka huu hakijafungua tu lango la ghadhabu, lakini pia ilifungua tena makovu ya siku za nyuma na kuwalazimisha wahindi kuuliza tena maswali magumu kuhusu utamaduni wa ubakaji, ugonjwa ambao umekuwepo kwa muda mrefu.

Katika mwezi uliopita, matukio muhimu yamefanyika nchini India. La kwanza, Mahakama Kuu ya India imeanza kusikiliza kesi ya Kolkata na Ofisi Kuu ya Upelelezi (CBI) imechukua mamlaka juu ya suala hilo.

Wakati huo huo, mahakama ya wilaya ya Siliguri (katika Bengal Kaskazini) imetangaza hukumu ya hatia katika kesi ya ubakaji na mauaji iliyotokea katika eneo la Matigara takriban mwaka mmoja uliopita, ambapo mhusika alihukumiwa kifo.

Zaidi ya hayo, kesi zaidi za ubakaji zinaendelea kuripotiwa kote nchini, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa mwanamke mchana huko Ujjain, Madhya Pradesh, na ubakaji na mauaji ya msichana wa miaka 14 wa Dalit huko Bihar.

Kutokana na matukio haya yote yanayofuatana, ni sawa kuhitimisha kwamba India iko katika hali ngumu na ya kufadhaisha, kuna mambo mawili yana ukweli.

Kwanza, kwamba taratibu za kutii sheria zipo, mahakama inafanya kazi kuelekea kutoa haki, na hukumu na adhabu hutamkwa na kutekelezwa.

Pili, ukatili wa kijinsia na ubakaji bado unaendelea. Kwa hivyo tatizo ni nini, na kwa nini India haiwezi kulitatua? Yaliyotokea hivi karibu huenda ikawa na majibu.

Mnamo Disemba 16, 2012, mwanafunzi wa tibamaungo mwenye umri wa miaka 23 alibakwa na wanaume sita katika basi lililokuwa likielekea huko New Delhi.

Muathirika, aliyepewa jina la utani Nirbhaya, au asiyeogopa, katika ripoti za vyombo vya habari, kwa sababu sheria ya India inakataza kumtaja muathirika wa ubakaji kwa jina lake la kweli, alikufa kwa majeraha siku chache baada ya shambulio hilo.

Uhalifu huo ulikuwa ni unyanyasaji wa kijinsia ambao ulileta mawimbi ya mshtuko kote nchini na kusababisha hasira kubwa kwa miezi kadhaa na kuvutia hisia za kimataifa na kusababisha mabadiliko makubwa, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa sheria mpya ya kupinga ubakaji ambayo inaweka vikwazo vya adhabu ya kifo kwa uhalifu huo.

Wanaume wanne waliohukumiwa walipatikana na hatia na kunyongwa mnamo Machi 20, 2020 katika jela ya Tihar.

Wa tano alijiua wakati akitumikia kifungo na huku mhalifu mwenye umri mdogo ambaye alikuwa chini ya umri wa miaka 18 wakati wa uhalifu aliachiliwa baada ya kifungo cha miaka mitatu, akihudumia kiwango cha juu chini ya sheria ya watoto nchini India.

Kulingana na ripoti ya ofisi ya kitaifa ya Uhalifu (NCRB), ambayo ilitoa takwimu 2022 za uhalifu mwishoni mwa 2023, India ilishuhudia kuongezeka kwa asilimia nne ya uhalifu dhidi ya wanawake ikiwa ni pamoja na ubakaji, mauaji, vifo vya mahari, unyanyasaji na mashambulizi ya tindikali.

Mnamo 2020, kulikuwa na kesi 371,503 zilizosajiliwa za uhalifu dhidi ya wanawake. Tangu wakati huo, kumekuwa na ongezeko la kutisha la viwango vya uhalifu huku kesi 445,256 zikiorodheshwa mnamo 2022.

Kesi za ubakaji zilizosajiliwa mwaka wa 2021 zilifikia 31,677, au wastani wa kesi 87 kwa siku  ongezeko la asilimia 19.34 kutoka 2020.

Hasa, hukumu zinazohusiana na ubakaji zilizosajiliwa kati ya 2018-2022 ni asilimia 28 pekee.

Mwaka jana, taasisi ya ‘Georgetown Women, Peace and Security Index’, iliorodhesha India vibaya, na kuiweka katika nafasi ya 128 kati ya nchi 177 katika masuala ya usalama, haki na ushirikishwaji wa wanawake.

Zaidi ya hayo, kuna ucheleweshaji wa taarifa za polisi na usajili wa malalamiko, na hivyo kuzuia utekelezaji wa haraka wa sheria zilizopo dhidi ya makosa ya ngono.

Ni safari ndefu hadi pale utamaduni wa kukabiliana uhalifu huo na ambao hatimaye unaweza kushinda mfumo dume, nguvu za kiume zenye sumu na chuki dhidi ya wanawake nchini India.

Huku kilele cha maandamano ya Kolkata, ni wakati mwafaka wa kuchukua mafunzo kutoka zamani ili kusuluhisha tatizo lililokithiri la uhalifu wa kijinsia katika kila ngazi ya kijamii, kukuza na kuhimiza mazingira yanayozingatia jinsia na usalama wa mazingira.

Vinginevyo, kufanya mabadiliko makubwa chini ya mfumo wa haki ya jinai au kwa sheria kunaweza kufanya kazi kwa muda tu.