RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema marehemu Cleopa David Msuya, alikuwa zawadi sio kwa jamii na familia yake, bali kwa taifa, akimtaja kuwa mzalendo na mwana halisi wa Tanzania.
Akizungumza katika ibada mazishi ya kiongozi huyo yaliyofanyika kijijini kwao Usangi, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro jana, alisema marehemu atakumbukwa kwa mambo mengi ikiwemo kujitolea maisha yake yote katika kuwatumikia Watanzania.
Alisema katika nyadhifa mbalimbali alizoshika aliweka rekodi mbili kubwa; kuwa Waziri aliehudumu katika wadhifa wa Wizara ya Fedha kwa kipindi kirefu zaidi kwa nyakati tofauti.
Alisema kuwa mtanzania wa mwisho kushika wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu kabla ya Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi ambapo sasa Makamu wa Rais anapatikana kupitia mgombea mwenza.
Alisema marehemu Msuya alikuwa na mchango mkubwa katika kutafuta fedha kwa ajili ya harakati za ukombozi za Kusini mwa Afrika.
Dk. Samia alisema marehemu alikuwa miongoni mwa viongozi waliokwenda China kwa ajili ya kutafuta fedha za ujenzi wa mradi wa reli ya TAZARA uliosaidia harakati za ukombozi na unaoendelea kunufaisha kiuchumi.
“Hiki kilikuwa kipindi kigumu cha kukabiliana na ushindani na shinikizo kutoka wafadhili wa kimataifa, wanasiasa nchini, wafanyabiashara na makundi mengine, baadhi yao wakiunga mkono mageuzi hayo na wengine wakiyapinga,” alisema.
Hata hivyo, alisema licha ya changamoto hizo, serikali ilifanikiwa kutatua shida kubwa zilizowakabili wananchi kama uhaba wa bidhaa muhimu na mfumko wa bei.
Alisema hata baada ya kustaafu, Msuya aliendelea kutoa mchango kwa maendeleo ya taifa kupitia ushauri wake kwa viongozi walio serikalini.
Alisema hadithi ya Msuya ilikuwa na mambo mengi ambayo viongozi wanapaswa kujifunza ikiwemo kupenda maendeleo na kutoacha kusimamia wanachokiamini bila kuyumbishwa.
Alisema marehemu Msuya aliamini kuwa ujuzi na utaalamu una nafasi kubwa katika kuleta maendeleo na aliheshimu maoni na ushauri wa kitaalamu.
Alisema serikali itaendelea kutumia busara na ushauri wake na wazee wengine katika ujenzi wa taifa.
Aliiomba familia na wote walioguswa na msiba huo kuendelea kumuombea na kujiombea binafsi ili Mwenyezi Mungu awafariji na kuwapa khatma njema.
Mapema Rais mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, akimzungumzia marehemu, alisema alikuwa mwalimu na mshauri mzuri, uwezo mkubwa wa uongozi, umakini wa kujenga hoja, uhodari wa kujieleza na kufafanua jambo gumu kuelekewa kwa urahisi hata kwa mtu asie mtaalamu wa uchumi na fedha.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa, alisema marehemu alikuwa na hekima, busara na upendo, ambaye alijitahidi kuwa na amani na watu wote.
Kwa upande wake, mtoto wa marehemu, Job Msuya, akizungumza kwa niaba ya familia, alieleza jinsi alivyomfahamu baba yake kama mlezi mwenye msimamo mkali wa kuwajengea watoto wake kujitegemea.
“Katika miaka yangu 54 niliyoishi na baba yangu, jambo kubwa nililojifunza kutoka kwake ni jinsi ya kupambana na kujitegemea, sikumbuki kama baba aliwahi kunipa hata senti moja kwenye mambo yangu binafsi,” alisema.
Alifafanua kuwa aliwasisitiza watoto wake wajifunze kupambana wenyewe, ingawa hakuwahi kukosa muda wa kuwashauri na kuwasaidia kwa ushauri wa kina walipopitia changamoto.
“Tulikuwa tunapata muda wa kuchambua changamoto tulizokuwa tukizipata, lakini pesa hakuwahi kunipa hata siku moja. Huo ndio msingi aliotufundisha – kujitegemea na kusimama wenyewe,” alieleza.
Msuya alifariki dunia Mei 7 katika hospitali ya Mzena Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo.
Viongozi mbalimbali walishiriki maziko yake akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.