IDADI ya watu wasio amini uwepo wa Mwenyezi Mungu duniani, wasio amini maisha baada ya kifo na wasio amini hakuna kuzaliwa upya baada ya kufa inaongezeka kwa kasi ulimwenguni.
Hatua ya kukana uwepo wa Mungu inaonekana wazi katika baadhi ya nchi na kwamba jambo hilo limekuwepo kwa muda mrefu miongoni mwa jamii mbalimbali hapa duniani.
Profesa wa sosholojia katika Chuo cha Pitzer, Claremont kilichopo jijini California nchini Marekani, Phil Zuckerman akielezea suala hilo aliwahi kusema kuwa kuna watu wengi wasioamini Mungu hasa katika zama hizi, kuliko wakati mwingine wowote.
Kulingana na utafiti uliofanywa katika nchi 57 na taasisi ya Gallup International, umebaini kuwa idadi ya watu wanaoamini dini imepungua kutoka asilimia 77 hadi asilimia 68 baina ya mwaka wa 2005 hadi mwaka 2011.
Aidha utafiti huo umebaini kuwa idadi ya watu wanaodai hawaamini Mungu imeongezeka kwa asilimia tatu, ambapo inakadiriwa kuwa jumla ya idadi ya watu wasioamini Mungu duniani ni asilimia 13.
Ni vigumu kutabiri kuhusu siku zijazo, lakini kwa kuzingatia tathmini ya kipimo kwamba kwa nini watu wengine walianza kuiamini na kwa nini wengine waliiacha, kinachoweza kuelezwa ni kutoa vidokezo juu ya nini kitatokea miongo ijayo.
Suali kubwa liliopo ni kwamba je kutakuwa na uhusiano gani baina ya wanadamu na Mungu kwenye karne zijazo?
Invyoonekana moja ya sababu za watu kufuata dini ni hutoa usalama katika ulimwengu, hata hivyo usalama huo huonekana kwamba sio wa uhakika.
Kutokana na hali hiyo haishangazi kuona nchi zinazowapa raia wake usalama mkubwa wa kiuchumi, kisiasa zina idadi kubwa ya wasioamini Mungu.
Kwa mfano katika nchi za Japani, Uingereza, Korea Kusini, Uholanzi, Jamhuri ya Czech, Estonia, Ujerumani, Ufaransa na Uruguay ni nchi ambazo dini ilikuwa muhimu sana kwenye karne moja iliyopita.
Hata hivyo, hivi sasa waumini wa dini katika mataifa hayo wamepungua, ambapo kupungua kwa waumini wa dini kunahusishwa na mifumo mizuri ya elimu na usalama wa kijamii.
Mwanasaikolojia Quentin Atkinson kutoka katika Chuo Kikuu cha Auckland kilichopo nchini New Zealand, alisema kuwa katika nchi zote tajiri hapa ulimwenguni imani ya dini inaonekana kupungua katika nchi nyingi ambazo zilishika dini, ikiwa ni pamoja na nchi kama Brazili, Jamaica na Ireland.
Marekani ni nchi moja kati ya nchi tajiri yenye kiwango cha juu sana cha dini, hata hivyo katika utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na taasisi ya Pew, uligundua idadi ya wamarekani wanaodai hawaamini Mungu imeongezeka kutoka asilimia 1.6 hadi asilimia 2.4 baina ya mwaka 2007 na 2012.
Ara Norenzyan, mwanasaikolojia wa kijamii katika Chuo Kikuu cha British Columbia huko Vancouver, Canada na mwandishi wa kitabu cha ‘Big God’, anasema kupungua kwa idadi ya waumini haimaanishi kutoweka kwa dini. Kila kitu kinaweza kubadilika muda wowote.
Hata ikiwa matatizo yote ya ulimwengu yangetatuliwa kimuujiza na sote tukaishi maisha ya amani, bado dini zingekuwepo. Hiyo ni kwa sababu inaonekana kuna uhusiano wa Mungu na wanadamu.
Moja ya mfumo wetu wa kufikiri, ni ule unaoturuhusu kuzungumza lugha ya awali, na huwapa watoto uwezo wa kutambua wazazi na kutofautisha kati ya vitu vilivyo hai na visivyo hai. Pia mfumo huo unatutia moyo kuelewa ulimwengu.
Wasomi wanaamini mfumo huu huiwezesha dini kujiendeleza yenyewe, pamoja na kusaidia kushinda hatari. Vilevile, unatuongoza kuhisi kuwepo kwa vitu visivyoonekana.
Wasioamini Mungu wanapaswa kupigana dhidi ya imani za kitamaduni na za kimageuzi. Wanadamu hupenda kuamini kwamba wao ni sehemu ya uumbaji na maisha yana maana na akili zetu hutafuta uazi.
Watu wengi wasioamini Mungu hutafuta usaidizi wa sayansi ili kuelewa ulimwengu na asili, lakini sayansi si nyepesi wakati wote kutoa ushuhuda kamili wa kile wanachokitafuta.
Inakadiriwa kuwa ailimia 20 ya wamarekani hawaendi kanisani, lakini asilimia 68 wanasema bado wanaamini Mungu na asilimia 37 wanajiona ni watu wa kiroho. Wanaamini kuna nguvu fulani ya kimungu huongoza ulimwengu.
Hivyo hivyo, watu wengi wanaodai kutomuamini Mungu bado wanaamini kuhusu mizimu, unajimu, karama au kuzaliwa upya katika mwili mwingine baada ya kufa.
“Watu wengi katika nchi za Scandinavia wanasema hawamwamini Mungu, lakini imani za kishirikina zinaaminiwa kuliko tunavyofikiri,” anasema Norenzyn.
Mbali na hayo, wasioamini Mungu hutegemea vitu kwa ajili ya kuwaongoza kimaadili katika maisha yao. Hii inathibitishwa na kuongezeka kwa wafuasi wa uchawi huko Marekani na upagani unaonekana kuwa dini inayokua kwa kasi zaidi nchini Uingereza.
Mbali na hilo, dini huhimiza umoja na ushirikiano. Hofu ya Mungu huenda ilisaidia kudumisha utulivu katika jamii za kale.
Atkinson anasema, “dhana juu ya adhabu – ikiwa kila mtu anaamini adhabu ni ya kweli, inaweza kutokea kwa jamii nzima. Katika hali kama hiyo kudumisha dini na kanuni kali za maadili linaweza kuwa ni jukumu muhimu sana.’
Joseph Bulbulia wa Chuo Kikuu cha Victoria cha Wellington huko New Zealand na wenzake waligundua katika utafiti wa makumi ya nchi, kuwa watu katika nchi masikini zenye hali mbaya, wana imani zaidi juu ya Mungu.
Vilevile, kuna hesabu rahisi nyuma ya kuenea kwa dini. Ulimwenguni kote, watu walio na dini wana watoto wengi zaidi kuliko watu wasio na dini, kuna ushahidi wa hilo,” anasema Norenzyan.
Pia ni ukweli kwamba watoto huwafuata wazazi wao linapokuja suala la kuamua kuwa wafuasi wa dini au la. Katika mazingira hayo ulimwengu usio na dini kabisa linaonekana ni jambo lisilo wezekana.
Kwa sababu za kisaikolojia, neva, kihistoria, kitamaduni – wataalam wanaamini dini haitakufa kamwe. Iwe dini inafuatwa kwa sababu ya upendo au hofu, imefanikiwa sana kudumisha uwepo kwake.
Zuckerman anasema, “Licha ya maumivu na mateso, mwanadamu anahitaji kupumzika, na watu wengi lazima wafikiri kuna kitu zaidi ya maisha, kiumbe kisichoonekana ambacho kinawapenda. Sitashangaa ikiwa wanao amini ni wengi zaidi ya wasio amini.”