Skip to content

Lookman, Osimhen waibeba Nigeria

ABUJA, Nigeria

NIGERIA imeanza kampeni yake ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) kwa ushindi mnono dhidi ya Benin huku Cameroun ikailaza Namibia nayo Mauritania ikishinda nyumbani dhidi ya Botswana juzi.

Washambuliaji, Ademola Lookman na Victor Osimhen walikuwa nyota wakati Nigeria ilipoishinda Jamhuri ya Benin magoli 3-0 kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio.

Nigeria walitawala tangu mwanzo, huku Lookman akitangulia kufunga katika kipindi cha kwanza kabla ya bao zuri la Osimhen kuongeza uongozi.

Lookman alifunga ushindi huo kwa bao la tatu, na kuwahakikishia Super Eagles kuondoka kifua mbele.

Mshambuliaji huyo alianza kufunga kunako dakika ya 23, akionyesha utulivu na ustadi mbele ya lango.

Safu ya ulinzi ya Benin ilijitahidi kuzuia mashambulizi ya Nigeria huku Osimhen akifunga bao la pili kwa shuti kali la kipekee katika dakika ya 55.

Bao lake lilifanya umati wa watu kuwa na mshangao, onyesho la kawaida la uwezo wake wa kumalizia.

Mechi ilipoendelea, ‘Cheetah’ wa Benin hawakuweza kupata jibu, na Lookman akaongeza bao lake la pili jioni katika dakika ya 78, akiimarisha uongozi wa Nigeria.

Super Eagles walisalia katika udhibiti muda wote, wakidumisha kutoruhusu bao na kupata alama tatu muhimu.

Katika mechi nyengine, Cameroun iliilaza Namibia 1-0, bao la pekee la Vincent Aboubakar lilihakikisha ushindi wa miamba hiyo mjini Garoua.

‘Simba Wasiofugika’ walilazimishwa kufanya kazi kwa bidii kusaka ushindi huo, huku Namibia ikitoa mtihani mkali. Aboubakar alifunga dakika ya 65, akipiga shuti lililorudi baada ya shuti la Bryan Mbeumo kupanguliwa.

Licha ya nafasi zaidi kwa pande zote mbili, matokeo yalisalia 1-0, na kuwapa Cameroun mwanzo mzuri wa kampeni yao ya kufuzu.

Wakati huo huo, huko Nouakchott, Mauritania ilipata ushindi wa 1-0 dakika ya mwisho dhidi ya Botswana.

Bao la dakika ya 84 la Sidi Amar liliwapa ‘Mourabitounes’ ushindi muhimu ili kuanza kampeni yao ya kufuzu AFCON.

Mechi hiyo ilikuwa ya ngome, huku Mauritania ikimiliki mpira, lakini, ikijitahidi kuvunja safu ya ulinzi ya Botswana.

Mauritania hatimaye walipata mafanikio wakati Beyatt Lekoueiry alipomtengeza Amar, ambaye aliachia shuti kali kwenye kona ya juu.

Kwengineko,Senegal, mabingwa wa AFCON 2021, walijikuta katika nafasi yenye changamoto isiyotarajiwa baada ya sare ya kushtukiza ya 1-1 nyumbani dhidi ya Burkina Faso.

Simba wa Teranga watakuwa na hamu ya kurejea watakapomenyana na Burundi, ambao kwa sasa wanaongoza kundi ‘L’ baada ya ushindi mnono wa mabao 3-2 ugenini dhidi ya Malawi.

Meneja wa Senegal, Aliou Cisse, atatafuta nyota kama Sadio Mane kuongoza katika kile kinachoahidi kuwa pambano muhimu kwa mabingwa hao watetezi. “Tunajua umuhimu wa mechi hii,” alisema, Cisse.

Burundi, inayoongoza kundi ‘L’ kwa sasa, haitakuwa na msukumo wowote, baada ya kuonyesha uthabiti katika ushindi wao wa ufunguzi.

Ghana, ambayo bado inayumbishwa na kichapo cha 1-0 kutoka kwa Angola, inakabiliwa na hali ya lazima ishinde dhidi ya Niger.

Kocha wa Black Stars, Otto Addo, atakuwa kwenye shinikizo la kutoa matokeo na kufufua kampeni ya kufuzu ya Ghana.(Goal).