JESHI la Magereza limesema litahakikisha wafungwa wenye sifa za kisheria wanashiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu, Kwa maelekezo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Aidha wanaendelea na utekelezaji wa maamuzi ya Bodi ya Parole kwa kupendekeza kwa Waziri Mambo ya Ndani kuachiwa kwa wafungwa 163 wakiwemo wanawake 11.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Jeremiah Katungu, alisema hatua hizo mbili zinadhihirisha dhamira ya serikali kuendeleza haki za msingi za binadamu, ikiwemo haki ya kuchagua viongozi.
Alisema wafungwa 163 wanaopendekezwa kuachiwa ni kati ya 206 wakiwemo wanawake 13 waliojadiliwa na bodi hiyo
“Wafungwa 43 wakiwemo wanawake wawili hawakupendekezwa kutokana na sababu mbalimbali licha ya kujadiliwa,” alisema.
Alisema mfumo wa parole una manufaa kwa taifa, ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji wa magereza, kuruhusu jamii kushiriki katika mchakato wa urejeshaji wa nidhamu na kuimarisha mahusiano kati ya jamii na jeshi la magereza.
Aidha unafanya wafungwa kuungana tena na familia zao wakiwemo wake, waume, watoto, wazazi, ndugu na jamaa na kuimarisha upendo na mahusiano na kuwapa fursa ya kujishughulisha na shughuli za maendeleo.
Balozi Hamis Kagasheki, Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, alisema jamii inapaswa kutambua kuwa mfumo wa parole si tu njia ya kupunguza msongamano, bali ni chombo cha kurejesha utu, nidhamu na matumaini mapya kwa wale waliokwenda kinyume na sheria lakini wameonyesha mabadiliko chanya.
