NA MARYAM HASSAN
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuwa anaridhishwa na mageuzi yanayofanyika na muhimili wa mahakamajambo linalosaidia watendaji kufanya kazi zao kwa haraka.
Dk. Mwinyi alieleza hayo baada ya kuweka jiwe la msingi la Mahakama ya Mkoa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar na kueleza kuwa mageuzi hayo yanachochea kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.
Alifafanua kuwa, awali majengo ya mahakama yalikuwa na hali ngumu kwa sababu ya uchakavu na baadhi ya mahakama ikiwemo Mahakama ya Wete kutokuwa na hali ya kuridhisha.
Alisema ujenzi wa mahakama hiyo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa miradi wa majengo ya mahakama za mikoa yote ya zanzibar unatekelezwa kwa fedha za ndani.
“Tulipozungumza mara ya kwanza tulifikiria kutekeleza miradi hii kwa kuomba wahisani wetu lakini niliona tuanze kwa kutumia fedha zetu kwani tungesubiri tutumie njia hiyo tungechelewa”,alieleza Dk. Mwinyi.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kutoa fedha ili majengo hayo yakamilike harakakwa lengo la kuongeza kasi ya utendaji wa mahakama na wananchi kupata haki zao kwa wakati.
Dk. Mwinyi alisema kuwa kukamilika kwa majengo saba ya mahakama za mikoa ambazo ndani yake kutakuwa na mahakama za wilaya, mahakama za kadhi na ofisi za mawakili na wadau wengine wa muhimili huo kutaleta mageuzi makubwa katika sekta ya sheria nchini.
“Majengi na miundombinu hii bila shaka itaongeza kasi ya utendaji kazi wa mahakimu hivyo nataka kuwahakikishia kwamba tutaendelea kutoa fedha kukamilisha miradi hii ili kuimarisha huduma na mazingira bora ya kufanyia kazi”, alieleza Dk. Mwinyi.
Kuhusu jengo lilikuwa likituliwa na Mahakama Kuu ya Vuga, Dk. Mwinyi alisema litabaki chini ya mahakama kwa lengo la kuweka makumbusho ya mahakama.
Alifafanua kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha Mji Mkongwe unaendelea kuwa na umaridadi kwa miaka 100 ijayo.
Awali Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu, Kai Bashiru Mbarouk, alisema mageuzi yanayoendelea, yalianzishwa na Dk. Mwinyi kwa k,uwa ni ya muhimu katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi na wadau wa mahakama.
Alisema mageuzi hayo yamejikita katika uimarishaji wa miundombinu, teknolojia ya habari na ushirikishwaji wa wadau wa mahakama.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla, alishukuru serikali kwa kutoa fedha zilizowezesha ujenzi wa majengo saba ya mahakama za mikoa unguja na pemba.
Alieleza kuwa majengo hayo yatakayokuwa na vifaa vya kisasa, yataimarisha utendaji wa muhimili huo na kwamba wanakusudia kujenga majengo mengine, ya Mahakama ya Rushwa na uhujumu uchumi, Mahakama ya Biashara, Mahakama ya Kadhi, na Mahakama ya Wilaya ya Makunduchi.
Akitoa salamu za wananchi wa Mkoa wa Mjini Unguja, Mkuu wa mkoa huo, Idrissa Kitwana Mustafa, alisema kasi ya utoaji hukumu inaridhisha lakini aliwataka watendaji kuongeza kasi hasa katika kesi za udhalilishaji.