WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka wafamasia nchini kutoa dawa kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao na kuacha tabia ya kutoa dawa kiholela, ili kuimarisha ufanisi wa huduma za afya na kuwalinda wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya dawa yasiyo sahihi.
Aliyasema hayo alipofungua kongamano la kisayansi na mkutano mkuu wa 54 wa Chama cha Wafamasia Tanzania, ambapo aliwataka watumie ujuzi na utaalamu wao kuwapa wahitaji dawa sahihi na kwa kuzingatia vipimo na maelekezo ya madaktari.
“Watanzania wenzangu, wakati umefika wa kuacha kutumia dawa pasipo ushauri wa watalamu wa afya. Nendeni vituo vya kutolea huduma za afya mpate vipimo na maelekezo sahihi ya matumizi ya dawa. Pia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba simamieni matumizi sahihi ya dawa hasa za antibiotics,” alisema.
Aliongeza kuwa suala hilo liende sambamba na kusimamia vizuri huduma za utoaji dawa katika maduka ya dawa na kuhakikisha madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya dawa na vifaa tiba yanadhibitiwa kwa ukaribu.
Aliitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba kuongeza udhibiti wa upotevu wa dawa, hususan katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma.
“Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI tumieni mifumo iliyopo katika kuziba mianya ya upotevu dawa vituoni na upatikanaji wa maoteo sahihi ya dawa ili kuepuka dawa kuharibika,” aliongeza.
Alitumia fursa hiyo kutaja jitihada zinazochukuliwa na serikali kuimarisha huduma za dawa kuwa ni pamoja na kuendelea kutoa fedha shilingi bilioni 16 kila mwezi kwa ajili ya dawa, hatua ambayo imeimarisha upatikanaji wa dawa hadi kufikia wastani wa asilimia 85.
Alisema serikali katika kuhakikisha nchi inaimarisha uwezo wa uzalishaji wa dawa na bidhaa nyingine za afya, imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji ambapo kwa sasa kuna viwanda 17 vya dawa, 75 vya vifaa tiba na 57 vya kutengeneza gesitiba.
Katika hatua nyingine, Majaliwa aliitaka Wizara ya Afya na Bohari Kuu ya Dawa kuiangalia upya sheria ya uagizaji wa dawa nchini kama inakidhi mahitaji ya sasa kwa kuwa inataka kutumia muagizaji mmoja.
“Ninataka mje mnishawishi ni kwanini tusiipeleke sheria hii bungeni tuibadilishe ili tuwe na waagizaji zaidi ya mmoja, kwa kuwa tunakwenda kuanzisha bima ya afya kwa wote tunahitaji dawa mpaka zahanati, hivyo muagizaji mmoja hatatosha,” alisema.
Kwa upande, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, aliwataka wafamasia kuhakikisha wanapotumia vyeti vyao katika uanzishaji wa maduka ya dawa wabaki kufanya kazi katika maduka hayo ili kuwezesha usimamizi mzuri badala ya kuweka vyeti na kuondoka.
Awali, Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania, Fadhili Hesekiah, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo afya.