Skip to content

Makachu kivutio kwa watalii –Soraga 

ABOUD MAHMOUD NA KHAMISUU ABDALLAH

WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga,amesema vijana wanaopiga makachu katika eneo la Forodhani, wamekua kivutio kikubwa cha utalii wakionyesha ustadi wao huo kwa wageni wanaoitembelea Zanzibar.

Soraga aliyasema hayo wakati akijibu suali la msingi lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir alietaka kujua kwa kiasi gani vijana hao wanaendelea kuitangaza Zanzibar kupitia sekta ya utalii.

Alisema mtindo huo wa kipekee wa sanaa siyo kutoka burudani peke yake bali unawavutia watalii na kuchangia katika kutangaza tamaduni za Zanzibar kimataifa.

Soraga alieleza kuwa kupitia mitandao ya kijamii, video na picha za vijana hao zimeeneza na kupeleka jina la Zanzibar mbali zaidi na kuwa sehemu ya urithi wa kipekee unaoelezea uzuri wa kisiwa hicho.

“Vijana wa makachu wamevutia wageni mashuhuri wengi, wakiwemo watu maarufu duniani kutoka kwenye sekta za burudani, siasa, michezo pamoja na wageni mashuhuri ambao wamevutiwa na sanaa hiyo,pamoja na wasanii wa kimataifa,wanamitindo na hata viongozi wa kitaifa na kimataifa ambao wameweka nia ya kutembelea kisiwa hichi,”alisema.

Aidha Waziri huyo alieleza kuwa wizara kupitia Mamlaka ya Mji Mkongwe inawatambua vijana hao rasmi na imeshafanya uchaguzi wa uongozi wa kikundi hicho.

Pia alisema Mamlaka inaimarisha usalama wawapiga makachu hao kwa kueka mstari maalum katika ukuta wa Forodhani ili kufahamu kina cha maji kilicho salama kwa kuogelea.

Sambamba na hayo alisema Mamlaka tayari imeatoa muongozo kwa vijana hao katika kuimarisha usafi wa eneo hilo pamoja na kulinda mila na silka za kizanzibari.