NEW YORK, UMOJA WA MATAIFA
MAREKANI imepinga rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotaka kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza, na kukosolewa vikali na wengi wa wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Rasimu hiyo iliyowasilishwa na wajumbe 10 wasio wa kudumu wa baraza hilo, ilitaka kusitishwa kwa mapigano mara moja, bila masharti pamoja na kuachiliwa huru mara moja mateka wote bila masharti.
Baraza hilo lenye wanachama 15 lilipiga kura 14-1 kuunga mkono azimio hilo, na Marekani ilitumia kura yake ya turufu kama mjumbe wa kudumu wa baraza hilo kulizuia.
Akizungumza baada ya kura hiyo, Robert Wood, naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, alisema kuwa Washington imeweka wazi kuwa itaunga mkono tu azimio ambalo linatoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa mateka kama sehemu ya usitishaji vita.
“Azimio hilo lingetuma ujumbe wa hatari kwa Hamas kwamba hakukuwa na haja ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo,” alisema.
Hatua ya Marekani ya kuzuia azimio hilo ilizua shutuma kali kutoka kwa wanachama wengi.
Mwakilishi wa kudumu wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia, alisema “inashangaza” kwamba Marekani ilipiga kura ya turufu katika juhudi za kuokoa maisha ya Wapalestina na Waisraeli, ingawa “hatupaswi kushangaa.”
Alisikitika kuwa kwa muda wa miezi kadhaa, Marekani imekuwa ikizuia na kusimama katika njia ya hatua ya baraza hilo kushughulikia hali mbaya ya Gaza na kuegemea upande mmoja wa mzozo huo ili kuendeleza malengo yake ya kisiasa kwa kugharimu maisha ya Wapalestina.
“Ni siku ya huzuni kwa Baraza la Usalama, kwa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla,” Balozi wa Algeria, Amar Bendjama aliwaambia wajumbe wa baraza hilo.