Skip to content

Othman: Jamii izingatie haki za watu wenye ulemavu  

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ameihimiza jamii kuzingatia haki kwa watu wenye ulemavu ili kuwajengea mazingira bora ya maisha na kutoa fursa sawa ya kukuza, kuimarisha na kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Othman aliyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani, yaliyofanyika viwanja vya Gombani ya Kale, wilaya ya Chake Chake, Pemba.

Alisema kufanya hivyo kunakwenda sambamba na kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema ‘Kukuza uongozi wa watu wenye ulemavu kwa mustakbali jumuishi na endelevu’, na inahimiza haki na fursa sawa kwa kundi hilo. 

 “Kaulimbiu hii inakwenda sambamba na Sheria ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Namba 8 ya Mwaka 2022 na pia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu wa Mwaka 2009 ambao Tanzania imeuridhia, kwa madhumuni ya kuutekeleza na yote haya ni katika azma ya serikali kuona kwamba hakuna anayeachwa nyuma katika maendeleo”, alieleza Othman. 

Aliongeza kuwa; “Tunafahamu kwamba watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo za kushindwa kupata baadhi ya haki zao. Hata hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau itahakikisha inakabiliana nazo au kuziondoa kabisa”.

Othman pia alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuzingatia upatikanaji wa haki hizo na kutekeleza kwa vitendo ujumbe wa mwaka huu uliobeba ajenda ya ushiriki na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu ili kukuza wigo wa kundi hilo katika nafasi za uongozi nchini.

Akitaja mambo yanayochangia ongezeko la watu wenye ulemavu, Othman alieleza kuwa ni ajali za barabarani pamoja na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza hivyo aliwaasa vijana wanaotumia vyombo vya moto wakiwemo waendesha bodaboda kuwa makini wanapokuwa barabarani.

Aidha kwa niaba ya serikali, aliwashukuru washirika wa maendeleo na wananchi waliojitokeza katika maadhimisho hayo, akisema kuwa hayo yote ni ishara ya umoja na upendo uliopo sasa, miongoni mwa Jamii za Watu wa Visiwa vya Unguja na Pemba. 

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hamza Hassan Juma, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Harusi Said Suleiman, alisema umoja na mshikamano wa jamii hutoa fursa muhimu kwa viongozi kutekeleza mipango na miradi ya maendeleo inayojengea mazingira bora yanayowasaidia wananchi.

Hivyo aliwahimiza wananchi wa Zanzibar, kuendelea kuwaunga mkono viongozi wakuu wa nchi na kujitokeza kwa wingi bila ya kujali itikadi zao za vyama kwani katiba ya nchi imeaweka misingi kwa wafuasi wa imani tofauti za kisiasa kufanyakazi pamoja kama njia muhimu ya kuimarisha amani, umoja na mshikamano.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadidi Rashid, alieleza kuwa ufanyika kwa maadhimisho hayo ni faraja na fursa kubwa nchini na duniani kote kwani kunaongeza hamasa, uelewa, uwezeshaji, kuwajali na kuwathamini watu wenye ulemavu ndani ya jamii zao na kote ulimewenguni.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Salma Saadat, alisema wao ni sehemu muhimu ya jamii na licha ya kuridhishwa kwao na hatua zinazochukuliwa na serikali zote mbili za tanzannia kutatua changamoto zao.

Akisoma risala ya  Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA), Haroub Soud Mzee, alieleza changamoto zinazowakabili, zikiwemo za upungufu wa vifaa saidizi na mafanikio yao yakiwemo ya ushiriki wao katika miradi ya maendeleo.

Aidha waliomba kuendelezwa na kuimarishwa kwa mazingira bora yatakayowapatia wepesi katika maisha ya kawaida zikiwemo kupata uteuzi wa nafasi za uongozi, uimarishwaji wa sera na sheria rafiki hasa wakati wa chaguzi na kutengewa fungu maalum la bajeti kwa jili ya watu wenye ulemavu mkubwa, sambamba na kuzisaidia Familia zinazoishi katika mazingira magumu.