Skip to content

Raia hawatoshika kiti cha urais Uganda – Jenerali Muhoozi

  • Afrika

KAMPALA, UGANDA

MKUU wa jeshi la Uganda, ambaye ni mtoto wa kiume wa rais Yoweri Museveni, jenerali Muhoozi Kainerugaba, amesema kwamba hakuna rais atakayeongoza Uganda na kwamba hilo ni jukumu la wanajeshi au polisi.

Muhoozi, ambaye siku chache zilizopita alinukuliwa akisema kuwa hatogombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2026, aliandika katika ujumbe kwenye mtandao wa X kwamba wanajeshi hawatawahi kuruhusu raia kuongoza taifa la Uganda.

“Hakuna raia ataongoza Uganda baada ya rais Yoweri Museveni. Maofisa wa usalama hawataruhusu hilo litokee. Raia ajaye atakuwa mwanajeshi au ofisa wa polisi”, alisema jenerali Muhoozi.

“Ningependa kutangaza kwamba asitagombea urais mwaka 2026,” ameandika Muhoozi kwenye mtandao wa X, akiongezea kwamba “Mungu ameniambia nishughulikie jeshi lake kwanza,” ameendela kuandika.

Muhoozi amesema ataunga mkono babake mwenye umri wa miaka 80. Museveni alichaguliwa kwa mhula wa sita madarakani katika uchaguzi uliokumbwa na ghasia na utata mwaka 2021, ambapo amekuwa madarakani tangu mwaka 1986.

Haijabainika wazi sababu ambazo zimepelekea Muhoozi kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2026 licha ya kuanza kampeni ya mapema na wafuasi wake wamekuwa wakiandandaa mikutano kote Uganda kumtayarisha kwa nafasi hiyo, baada ya kutangaza mwaka 2023 kwamba atagombea urais.

Amekuwa akijiita kuwa mtambo mbadala wa kuzalisha umeme akitumia neno la kiingereza ‘standby generator’ maana kwamba yuko tayari kuchukua uongozi wa nchi babake akiondoka madarakani.

Kinyang’anyiro cha urais mwaka 2026 kinatarajiwa kuvutia wagombea kadhaa ambao ni wanasiasa mashuhuri nchini Uganda ikiwa ni pamoja na Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine na Dk. Kiiza Besigye.

Muhoozi ameendelea kuandika kwamba ataendelea kuhudumu katika jeshi. “Hakuna kitu muhimu duniani zaidi ya kuhudumu katika jeshi la Uganda UPDF”, ameandika kwenye X.

Jenerali Muhoozi Kainerugaba aliteuliwa na babake kuwa mkuu wa majeshi ya Uganda UPDF. Kumekuwepo taarifa kwamba rais Yoweri Museveni anamtayarisha Muhoozi kumrithi baada yake kuondoka madarakani.