NA MWANAJUMA ABDI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema ameingia madarakani akiwa na utekelezaji wa falsafa ya R4, baada ya kubaini nchi imegawanyika kutokana na itikadi za kisiasa.
Hayo ameyasema jana wakati akifunga mkutano mkuu wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi kwa mwaka 2024, hafla iliyokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 60 tangu kuasisiwa kwa jeshi hilo, iliyofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Alisema falsafa ya R4 ambao ni pamoja na maridhiano, kustahamiliana, kubadilika na kujenga taifa, zina lengo la kuinganisha nchi jambo ambalo litaharakisha maendeleo.
Alisema wakati serikali inapotekeleza falsafa ya R4 sio kama wametupilia mbali utekelezwaji wa sheria za nchi au wameruhusu utovu wa nidhamu utokee ndani ya nchi.
Alisema sheria, mila, desturi zetu zipo pale pale miongozo ya kufanya mikutano na mengine yote ipo hivyo R4 ni falsafa ya kuja kuunganisha taifa na sio kuruhusu utovu wa nidhamu kama unavyofanywa na baadhi ya watu.
Dk. Samia alisema wakati serikali ikihangaika kusimamia umoja wa kitaifa, kuunganisha nchi kuwa kwenye utulivu wapo baadhi ya wengine wanakwenda kinyume na kuonya kuwa serikali haitovumilia vitendo vya kuleta mifarakano.
Alisema huu ni wakati mzuri kwa wanaoandaa machafuko wasisahamu mapito waliyopita, kwa vile falsafa hizo ndiyo iliyowarejesha.
“Kama sasa wameshaota mikia sheria zile zipo na sheria za mahuluki tabu pia zipo tutashuhulika nao R4, sio sababu ya utovu wa nidhamu sio sababu ya kuvunja sheria za nchi na sheria zipo pale pale”, alisema.
Alieleza serikali imejitahidi kurejesha uhuru wa vyama vya siasa, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wananchi kwa ujumla, wale waliokuwa uhamishoni walirejea nchini na waliokuwa na kesi za jinai zilifumbiwa macho, waliokuwa jela walitolewa na sasa wapo huru na wanaendelea na shughuli zao zikiwemo za siasa.
Samia alisema dhamana yake na vyombo vya ulinzi ni kulinda amani hivyo hatokuwa na muhali kwa yeyote anayetaka kuvuruga amani ya nchi, ambapo amewavumilia katika mengi lakini katika amani hatukuwa tayari kwa anayeratibu na hata anayefanya mipango hiyo miovu.
Aliliagiza jeshi la polisi lianze uhalifu katika mtandao, ambapo mabadiliko ya dunia wanayowazungumzia ni ongenezo la matumizi ya mitandao na akili bandia ambayo ni lazima waendelee kuyaangalia kwa jicho la karibu.
Alifahamisha kuwa kwa mujibu wa taarifa hiyo miongoni mwa uhalifu unaongezeka kwa kasi katika eneo hilo ni kutoa taarifa za uzushi na uongo, kusambaza picha za ngono na matusi na watu kunyanyasana ndani ya mitandao, ni wazi kwamba kutokana na maendeleo ya kiteknolojia hususani teknojia ya akili bandia, uhalifu wa kutoa taarifa za uzushi na uongo umeongezeka.
Alisema uchaguzi utapita lakini Tanzania itabakia, hivyo anataka kubakia Tanzania iliyosalama na yenye utulivu ili shughuli za maendeleo ziweze kuendelea.
Samia alilitaka jeshi la Polisi kuwa macho wakati wote kabla na baada ya uchaguzi, hivyo aliwasisitiza Polisi kuwa yeyote anayehatarisha amani ya nchi yetu kwa kisingizio za chaguzi hizo anachukuliwa hatua haraka na kufikishwa katika vyombo vya sheria.