RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua jitihada mbali mbali kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto.
Dk. Mwinyi alieleza hayo jana katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, wakati wa uzinduzi wa kitabu cha taarifa za kesi za udhalilishaji wa kijinsia kwa mwaka 2022 na 2023 uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni mjini Unguja.
Alieleza kuwa hatua hizo zinalenga kuhakikisha hatua madhubuti zinachukuliwa kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ili vitokomezwe kabisa huku akitaja baadhi ya jitihada hizo kuwa ni kuimarisha sheria za kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya vitendo hivyo.
Alitaja hatua nyengine kuwa ni kuanzishwa kwa mahakama maalum kwa ajili ya kesi za udhalilishaji katika mikoa yote ya Zanzibar iliyolenga kuhakikisha maamuzi yanatolewa ndani ya muda mfupi.
“Hatua nyengine ni kuundwa kwa Kamati ya kuzuia vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia yenye wajumbe 25, kutoka sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na taasisi za serikali, binafsi na dini. Kamati hii inalenga kutambua mianya ya udhalilishaji katika maeneo kama shule, hospitali, madrasa, na sehemu za utalii, na kutoa mikakati ya kuzuia vitendo hivyo”, alisema Dk. Mwinyi.
Aliongeza kuwa jitihada hizo zimeanza kuzaa matunda, ambapo idadi ya kesi za udhalilishaji imepungua kwa kiasi kikubwa hata hivyo alizitaka kamati hizo kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za udhalilishaji na njia za kupambana nao kwa vile kesi hizo zinaendelea kuripotiwa.
“Jitihada hizo za serikali zimeanza kuzaa matunda kwa kupungua matukio ya udhalilishaji kutoka kesi 432 zilizoripotiwa mwaka 2022 hadi kufikia kesi 348 zilizoripotiwa kwa mwaka 2023 na kushuka hadi kufikia kesi 289 kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba 2024”, alifafanua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar, Mgeni Jailan Jecha, alisema lengo la kitabu hicho ni kutoa taarifa sahihi kuhusu mwenendo wa kesi za udhalilishaji Zanzibar na kusaidia jamii kutambua hali halisi.
“Takribani mikoa yote ya Zanzibar imeshuhudia kupungua kwa kesi za udhalilishaji, isipokuwa mkoa wa Kusini Pemba, ambapo kulikuwa na ongezeko la asilimia 10.4 kati ya mwaka 2022 na 2023 na mkoa wa Mjini Magharibi bado unaongoza kwa idadi kubwa ya kesi, lakini pia umeonyesha kupungua kwa asilimia 11.7 katika kipindi hicho”, alieleza DPP Jecha.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Wanawake na Watoto, Riziki Pemba Juma, alisema vitendo vya udhalilishaji vinaendela kufanyika ndani ya zanzibar licha ya kupungua kwa matukio yanayoripotiwa.
Pembe alisema kesi nyingi za udhalilisha zinakosa hatia kutokana na upelelezi kuchukua muda mrefu kunakosababishwa na muhali uliopo ndani ya jamii kutoa ushahidi jambo linalochangia watuhumiwa wengi kuachiwa huru.
Alisema ushirikiano wa pamoja unahitajuka katika kupambana na kupinga vitendo vya udhalilishaji kwa kuwa tayari kutoa ushahidi Mahakamani na kushirikiana na taasisi husika katika kuhakikisha sheria inafuata mkondo wake na watuhumiwa wanahukumiwa kwa mujibu wa sheria.