Skip to content

Serikali yatenga bl.1,680 kulisha wagonjwa hospitali zote

WIZARA ya Afya inatenga jumla ya shilingi 1,680,000,000 kwa mwaka kwa ajili ya huduma za vyakula kwa kila hospitali za Wilaya Unguja na Pemba.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hassan Khamis Hafidh, alisema hayo katika Baraza la Wawakilishi wakati akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, Dk. Mohammed Ali Suleiman, aliyetaka kujua serikali imetenga kiasi gani cha fedha kwa mwaka kwa ajili ya huduma za vyakula katika hospitali za Wilaya na vipi fedha hizo zinagawanywa na kusimamiwa kwa kuhakikisha huduma bora kwa wagonjwa .

 Alisema Wizara imeunda kamati ya ukaguzi wa huduma zinazotolewa na kampuni binafsi, ili kuishauri wizara kwa changamoto mbalimbali zinazojitokeza ikiwemo kwenye huduma ya vyakula cha wagonjwa.

Aidha alisema ili kuhakikisha ubora wa chakula kwa wagonjwa wa hospityali hizo, Wizara imeagiza kampuni binafsi SAIFEE kuhakikisha ratiba ya mlo wa wagonjwa unalingana na muongozo wa jamii ya Zanzibar. 

Hata hivyo, alisema Wizara ya Afya Pemba, inakuwa na taratibu  wa kupita katika hospitali zote kwa kila kipindi, ili kusikiliza kero za wagonjwa hususan kwa upande wa vyakula na kuwashauri kampuni binafsi kutoa vyakula vinavyostahiki kwa wagonjwa ili kuboresha afya zao na kuondosha malalamiko. 

“Huduma za vyakula katika Hospitali za wilaya Micheweni, Kinyasini na Vitongoji zinasimamiwa na kampuni binafsi ya SAIFEE ambayo imeingia mkataba na serikali kupitia Wizara ya Afya na kuwapatia wagonjwa kulingana na mahitaji yao”, alisema.

Hata hivyo, alisema hospitali ya Abdalla Mzee wananunua chakula kulingana na fedha za matumizi ya Ofisi (OC) wanayopata na wanapanga matumizi yao wenyewe ya chakula na wanapeleka Wizarani kwa kulipwa.